Washitakiwa Wa Kesi Ya Wizi Wa Shilingi Bilioni 1.8/= katika akaunti ya madeni ya nje Farijara Hussein (Kushoto) Na binamu yake Rajabu Maranda (Kulia) wakiwa katika ulinzi mkali wa jeshi la Polisi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Juni 25, mwaka huu itamsomea maelezo ya awali ya Kada wa CCM, Rajabu Maranda na wenzake watano akiwamo Ajay Somani na ndugu yake Jai Somani wote wanakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh 5.9 bilioni za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Maranda na binamu yake Falijala Hussein wanatumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh 1.8 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Licha kusubiri kusomewa maelezo hayo ya awali, Maranda na Farijala Juni 26, mwaka huu wanatarajiwa kusomewa hukumu nyingine kwenye kesi ya wizi wa Sh 2.2 bilioni za EPA za BoT.Wakili wa Serikali, Alapha Msafiri jana, alidai mbele ya Hakimu Ritha Tarimo kuwa, kesi ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Baada ya kutoa maelezo hayo, Hakimu Tarimo alisema anaiahirisha hadi Juni 25, mwaka huu kwa sababu hakimu anayeisikiliza Hakimu Mfawidhi, Alvin Mgeta hayupo.
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Maranda, Farijala Hussein, Ajay Somani na ndugu yake Jai Somani pamoja na wafanyakazi wawili wa BoT, Ester Komu ambaye anadaiwa kuwa wakati wizi huo unafanyika alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Madeni na Bosco Kimela ambaye alikuwa Kaimu Katibu wa BoT.
Inadaiwa kuwa, washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama na kutenda makosa hayo kati ya Desemba 2004 na Mei 2005, jijini Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo, Maranda anakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kwa upande wa wafanyakazi wa BoT, wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kuisababishia benki hiyo hasara ya Sh 5.9 bilioni.
Maranda anadaiwa kughushi hati za uongo na kuziwasilisha katika Benki ya Baroda, akionyesha kuwa Thabit Mapunda ni mwanahisa wa Kampuni ya Liquidity Services Limited.
Ilidaiwa kuwa, kati ya Septemba 2 na Desemba 13 mwaka 2005, Maranda, Ajay na Jai walijipatia Sh 3,975,820,000 kutoka BoT baada ya kudanganya kuwa Kampuni ya Liquidity, imepewa deni na Kampuni ya M/S Societe Alsacienne De Construction De Machines Textiles ya Ufaransa.
Ilidaiwa kuwa kati ya Septemba 2 na Desemba 13 mwaka 2005, Maranda alijipatia Sh1,937,081,643 kutoka BoT, baada ya kudanganya kuwa,Kampuni ya Liquidity imepewa deni na Kampuni ya M/S Societe ya Ufaransa.
Pia, alidai kuwa Agosti 30 mwaka 2005, Komu na Kimela, wakiwa waajiriwa wa BoT waliisababishia benki hiyo hasara ya Sh5.9 bilioni.
Post your Comment