Katibu Mkuu mpya wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk.
Vicent Mashinji amewataka wananchi kumpima kwa kazi yake baada ya muda
mfupi na aliyekua Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa.
Akiongea
na waandishi wa habari hivi karibuni, Dk. Mashinji alisema kuwa ameweka
mikakati mipya ya kuisuka Chadema kuanzia ngazi ya vijiji na kwamba
kazi atakayoifanya itawapa nafasi Watanzania kumpima kama viatu vya Dk.
Slaa vimemtosha au vimempwaya.
Dk. Mashinji amesema kuwa moja kati
ya mikakati wanayokuja nayo ni kupunguza uanaharakati na kujiandaa
kuongoza Serikali. Ameongeza kuwa kupitia mikakati yao mipya, wanataka
Halmashauri zote zinazoongozwa na Chama Chao ziwe mfano wa kuigwa na
kuwapa matumaini watanzania kuwa wanaweza kuongoza na kuleta maendeleo
ya hali ya juu nchini.
Katika hatua nyingine, Dk. Mashinji
amekanusha kuwepo kwa upendeleo katika nafasi za Wabunge wa Viti Maalum.
Alifafanua kuwa nafasi zilitolewa kwa kila mkoa na kwamba walipanga
majina yote kwa kutumia vigezo stahiki.
“Hakuna upendeleo… na
kwenye Baraza Kuu wote waliokuwa wanalalamika walikuwa wanajua, japokuwa
kuna shinikizo la nje ya chama linaloingia ndani kuja kutuvuruga,”
alisema.
Alisema kuwa chama hicho hakitaacha kamwe sera yake ya kupinga ufisadi.
Post your Comment


