Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema inaendelea kumtafuta
Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwa ajili ya
kumhoji kuhusu mahubiri yake aliyoyatoa wiki moja iliyopita.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jeshi hilo bado linaendelea kumtafuta
na endapo mtu yeyote ana taarifa za alipo askofu huyo, asisite kupeleka
taarifa Polisi ili akamatwe.
Kamanda Sirro alisema Askofu Gwajima hajapatikana na hawafahamu
amekwenda wapi, lakini bado wanaendelea kumtafuta kwa mahojiano zaidi.
“Tunaendelea kumtafuta, tunaamini tutampata ili ahojiwe, tunawaomba pia
wananchi yeyote mwenye taarifa juu ya mahali alipo askofu huyo tunaomba
watupe taarifa ili aweze kukamatwa,” alisema Sirro.
Askofu Gwajima anatafutwa na jeshi hilo kwa ajili ya kuhojiwa juu ya
mahubiri yake aliyoyatoa Juni 11, mwaka huu kanisani kwake Ubungo Maji
jijini Dar es Salaam. Katika mahubiri hayo ambayo yalisambaa katika
mitandao mbalimbali ya kijamii, askofu huyo alisikika akiukosoa utendaji
kazi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Pia Gwajima alisikika akimshauri Rais John Magufuli, kuhama Chama Cha
Mapinduzi (CCM) iwapo watakataa kumkabidhi uenyekiti na kwamba apeleke
muswada bungeni, kuondoa kinga ili rais ashtakiwe kwa makosa
aliyoyafanya akiwa madarakani.
Post your Comment



