Marekani itatoa dola milioni 800 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Balozi
wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Mark Childress aliyekutana na kufanya
mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amesema kutolewa kwa fedha hizo ni uthibitisho kuwa kutotolewa
kwa fedha za awamu ya pili ya mradi wa changamoto za milenia (MCC-2)
hakujaondoa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Marekani ikiwemo
utoaji wa misaada ya maendeleo.
"Tumezungumza
mambo kadhaa, na wiki hii Tanzania na Marekani kupitia shirika letu la
misaada la USAID tunatarajia kutiliana saini mkataba wa zaidi ya dola
milioni 400 kwa ajili ya mwaka ujao, pia tumezungumza kuwa kutakuwa na
dola milioni 800 zitakazotolewa na Marekani kwa ajili ya miradi
mbalimbali na hii haihusiani na MCC.
"Ukweli
ni kwamba tunayo mengi ya kufanya pamoja katika sekta mbalimbali
zikiwemo afya, elimu na kilimo na tutafanya kila juhudi kuhakikisha haya
yanafanikiwa" Amesema Balozi Mark Childress muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo na Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amesema serikali yake ya awamu ya tano itaendeleza na
kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Marekani na kwamba fedha za
msaada kutoka Marekani ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania.
"Amekuja
kutuhakikishia kwamba watatoa hela kwa ajili ya Tanzania na anasema
sasa hivi watatoa zaidi ya dola milioni 800, na mkataba mwingine
tunaweza tukasaini hata kesho wa dola milioni 410, anasema kutotoa hela
za MCC hakuna maana kupotea kwa urafiki wa Tanzania na Marekani, urafiki
wa Tanzania na marekani upo pale pale na sasa wanaongeza hela nyingi
zaidi katika kuonesha kwamba juhudi za HAPA KAZI TU zinaendelea" amesema Rais Magufuli.
Wakati
huo huo Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Mhe. Didier Reynders Ikulu
Jijini Dar es salaam, ambapo viongozi hao wamezungumzia kuendeleza na
kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili hususani katika maendeleo.
Pamoja
na kuzungumzia miradi ya ushirikiano inayotekelezwa kati Tanzania na
Ubelgiji katika mkoa wa Kigoma, viongozi hao pia wamekubaliana kuongeza
ushirikiano katika biashara na uwekezaji ambapo Mhe. Didier Reynders
ameahidi kushawishi kampuni nyingi za Ubelgiji kuja kuwekeza hapa
nchini.
Katika
hatua nyingine Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Italia hapa nchini
Mheshimiwa Luigi Scotto ambaye amemaliza muda wake wa miaka mitatu.
Balozi
Luigi Scotto amesema katika kipindi chake amewezesha kuongezeka kwa
biashara kati ya Italy na Tanzania kwa asilimia 35 na ameielezea
Tanzania kuwa ni nchi nzuri aliyoipenda na kwamba ataendelea kutangaza
fursa zilizopo Tanzania huko Italia na kwingineko.
Mapema
leo asubuhi, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametia saini kitabu cha
maombelezo katika Ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Nchi za
Kiarabu ya Saharawi iliyopo Mikocheni Jijini Dar es salaam, kufuatia
kifo cha Rais wa nchi hiyo Mohamed Abdelaziz aliyefariki dunia Jumanne
iliyopita tarehe 31 Mei, 2016.
Rais
Magufuli ambaye amepokelewa na Balozi wa Saharawi hapa nchini Mhe.
Brahim Salem Buseif amesema Marehemu Mohamed Abdelaziz ambaye pia
alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Polisalio Front, atakumbwa kwa juhudi
zake za kupigania ukombozi na uhuru wa Saharawi.
"Kwa
niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania napenda kutoa salamu zangu za
pole kwa Serikali na wananchi wa Saharawi kwa kumpoteza kiongozi ambaye
alijitoa kwa ajili ya kupigania ukombozi na uhuru wa Jamhuri ya
Saharawi.
"Namuombea kwa Mwenyezi Mungu, aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina" Amesema Dkt. Magufuli katika salamu hizo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
06 Juni, 2016
Post your Comment



