MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na wenzake wanne ambao ni
madiwani wa Halmashauri ya Meru wilayani Arumeru, wamesomewa shitaka la
kuharibu uzio eneo la Leganga wilayani humo. Walisomewa shitaka lao
mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augustine
Rwezile jana.
Mwanasheria wa Serikali, Gaudensia Joseph alidai Nassari na wenzake
ambao ni Paulo Samuel, Japhet Joseph, Zephania Mwanuo na Anderson Sikawa
kwa pamoja na madiwani wenzao 24, ambao walisomewa shitaka lao awali
waliharibu uzio wa Naftani Makere.
Joseph alimuomba Hakimu Rwezile kuwaongeza washtakiwa hao watano
akiwemo Mbunge Nassari, ambapo awali katika shitaka lao linalowakabili
mahakamani hapo, hawakuwepo mahakamani kwa sababu mbalimbali. Alidai
wanashtakiwa kwa kuharibu uzio, Mei 4 mwaka huu, eneo la Leganga wilaya
ya Meru.
Alidai walisababisha hasara ya Sh milioni 7 kwa kuharibu uzio huo.
Wote walikana mashitaka. Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao ambao ni
Charles Abraham na Gift Joshua, waliomba dhamana kwa wateja wao.
Hakimu Rwezile alikubali ombi la wakili huyo kutoa masharti ya
dhamana ya kusaini Sh milioni moja na kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja.
Walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana.
Washtakiwa wengine waliofikishwa awali ni Mwenyekiti wa Halmashauri
ya Meru, Willy Njau (Chadema) na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,
Nelson William. Wengine ni Elisa Stephen, Digna John, Dina Erick, Wilson
Fanuel, Josephine Anael, Samuel Ismail, Agness Eliya, Isack Afitwe na
Neema Isack.
Washtakiwa wengine ni Gadiel Stanley, Jeremiah Masawe, Peter Efatha,
Benard Wilson, Henry Benjamin, Emanuel Pendael, Fadhila Joseph, Penzila
Palangyo, Mary Antony, Roman Laurance, Bryson Mosses, Franck Ngoye na
Eveline Julius. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 28 mwaka huu
itakapotajwa tena kwa kuwa upelelezi haujakamilika.
Post your Comment



