Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 10 Juni, 2016 amemuapisha Mhe. Jaji Shaaban Ali Lila kuwa Jaji wa
Mahakama ya Rufani, Ikulu Jijini Dar es salaam.
Kabla ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Jaji Shaaban Ali Lila alikuwa Jaji Kiongozi.Wakati huohuo, Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Jaji Ferdinand Leons Katipwa Wambali kuwa Jaji Kiongozi.
Kabla ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Jaji Kiongozi, Mhe. Jaji
Ferdinand Leons Katipwa Wambali alikuwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto, Mkoani Tanga.
Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Leons Katipwa Wambali amechukua nafasi
iliyoachwa wazi na Mhe. Jaji Shaaban Ali Lila ambaye amekua Jaji wa
Mahakama ya Rufani.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. John Pombe Magufuli
ameagana na Balozi wa Oman hapa nchini Mhe. Saoud Ali Mohamed al
Ruqaishi ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.
Akizungumza na Balozi huyo, Ikulu Jijini Dar es salaam Rais Magufuli
ameishukuru Oman kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano wa kihistoria na
kidugu na Tanzania, na ameahidi kuwa serikali yake ya awamu ya tano ipo
tayari kuongeza ushirikiano huo.
Mhe. Rais Magufuli pia amemuomba Balozi Saoud Ali Mohamed al Ruqaishi
kufikisha salamu zake kwa Sultani wa Oman Mtukufu Qaboos bin Said al
Said na kumueleza kuwa Tanzania inawakaribisha wawekezaji na
wafanyabiashara wa Oman na inatarajia kuona miradi ya ushirikiano katika
uwekezaji ukiwemo mradi wa Bagamoyo inaanza kutekelezwa haraka.
"Naomba umfikishie salamu zangu za dhati Mtukufu Qaboos
bin Said al Said, Sultan wa Oman na umwambie tunamkaribisha Tanzania na
nitafurahi kuona mradi wa uwekezaji wa Bagamoyo unakuwa kielezo cha
undugu na urafiki wetu uliodumu kwa miaka mingi" Amesema Rais Magufuli.
Tanzania kwa kushirikiana na nchi za Oman na China zimekubaliana kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo Mkoani Pwani.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
10 Juni, 2016
Post your Comment






