Serikali
imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 59. 5 katika Mwaka 2016/17 ili kupeleka
shilingi milioni 50 kwa kila kijiji ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi (CCM).
Hayo
yamesemwa leo Bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenister
Mhagama alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa
Ruvuma, Mhe. Jackiline Ngonyani aliyetaka kujua lini serikali itaanza
kutoa kiasi cha Tsh. Milioni 50 kwa kila kijiji au mtaa ili kuwasaidia
wananchi kuboresha mitaji yao.
“Fedha hizo
zitatolewa baada ya kukamilisha taratibu mahususi zinazolenga
kuhakikisha uwepo wa tija katika matumizi ya fedha hizo,”alisema
Mhagama.
Mhagama
alimuomba Mbunge huyo kusubiri utekelezaji wake kuanzia mwaka wa fedha
2016/17 mara baada ya kukamilika kwa mfumo wa muundo wa Utekelezaji wa
zoezi zima ambapo kazi imeanza kufanyika.
Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano inayo nia ya dhati ya kuwainua wananchi hasa wa kipato cha chini ili kukuza mitaji yao.
“Serikali
hii inatekeleza kwa vitendo kile inachokiahidi aliongeza Mhagama na
kuwataka waheshimiwa wabunge waeendelee kuiamini Serikalia yao ambayo
inafanya kazi kwa dhati kama ilivyo kauli mbiu ya mhe. Rais John Pombe
Magufuli ya “Hapa Kazi Tu”.
Post your Comment



