WABUNGE wamechachamalia hatua ya Serikali kutaka kiinua mgongo chao
wanachopaswa kulipwa baada ya miaka mitano ya kazi yao ya ubunge kitozwe
kodi na kusema kuwa uamuzi huo si sahihi kwa kuwa utaminya maslahi yao
na kulenga kuwasukuma kuwa ombaomba baada ya kustaafu kazi hiyo.
Aidha, imependekezwa kuwa, iwapo hakuna marekebisho yatakayofanywa na
Serikali kuhusu kodi hiyo, tozo hilo la kodi liwahusu pia viongozi wote
wa kisiasa, ili kuleta usawa katika maslahi.
Kama jinsi Kamati ya Bunge ya Bajeti ilivyowasilisha taarifa yake
Bungeni kuhusu hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2015/16, pamoja na
tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha
2016/17, wabunge hao wa Kambi ya Upinzani kupitia taarifa yao na wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), walisema hatua hiyo haikuwa na umuhimu wowote
kutajwa kipindi hiki, kwa sababu utekelezaji wake, ikiwa utapitishwa ni
mwaka 2020.
Akitoa maoni ya Kamati hiyo ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Hawa Ghasia ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, alisema kwa miaka mingi
Bunge limekuwa mstari wa mbele kujadili na kupendekeza watumishi wa
umma kusamehewa kodi kwenye malipo ya viinua mgongo wanavyolipwa.
“Bunge limekuwa likishauri hivi ukizingatia kuwa mishahara ya
watumishi wa umma na hata viongozi wa siasa imekuwa ikikatwa kodi, hivyo
hatua hii inayopendekezwa na Serikali inakuwa ‘double taxation’
(ikimaanisha kutozwa kodi mara mbili),” alisema.
Alisema ni muhimu Serikali ikafikiria suala hilo upya kurekebisha
kodi hiyo na kama iishindikana ijumuishe viongozi wote wa kisiasa na si
wabunge pekee. Wabunge mmoja mmoja wakichangia hoja akiwemo Mbunge wa
Mwibara, Kangi Lugola (CCM), aliyeeleza kuwa, hatua hiyo ya Serikali
haiwatakii mema kwa sababu imelenga kukipunguza hata kile kiasi kidogo
wanachojidundulizia kwa miaka mingi ili kiwasaidie wakati wakiwa
wamestaafu ubunge.
Kwa maelezo yake, fedha wanazopata ambazo Serikali inaziona kuwa
nyingi, huishia kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo, mara
nyingi wabunge huombwa kuchangia michango ya wananchi wanaopatwa
matatizo majimboni.
“Mheshimiwa Waziri wa Fedha anapaswa kufahamu kuwa sisi wabunge
mshahara wetu ni mdogo sana kuliko wake na hatuna pensheni. Anapaswa
kutambua kuwa, kule mitaani wabunge wamegeuzwa ATM kwa kuombwa fedha
karibu na kila mtu, hivyo kuhitaji kuachiwa kiinua mgongo chetu kama
kilivyo,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa wabunge ndio wanaopigania kila wakati mafao ya
watumishi wengine wa umma yasikatwe kodi, hivyo Serikali iliangalie tena
suala hili na kulifanyia marekebisho. Naye Mbunge wa Sikonge, Joseph
Kakunda (CCM), alisema, Ofisi ya Mbunge ni taasisi inayojitegemea na
kwamba fedha zinazoonekana nyingi si za mbunge, bali ni za jamii, hivyo
kukata kodi katika kiinua mgongo cha mbunge ni kumuumiza.
Kwa upande wa kambi ya Upinzani Bungeni, aliyewasilisha taarifa kwa
niaba ya Msemaji Mkuu ambaye ni Waziri Kivuli wa Fedha na Mbunge wa
Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde alisema,
Serikali haijawataja Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Wakuu wa Mikoa
na Wakuu wa Wilaya katika kundi la wanaopaswa kutozwa kodi ya kiinua
mgongo, badala yake imewabana wabunge pekee.
Alisema, “tuko tayari kutoa ushirikiano kwa serikali kupanua wigo wa
mapato kwa njia hiyo iwapo itawajumuisha viongozi hao iliowaacha.”
Wakati huo huo, wabunge hao wameshawishiana kutokubali kutumika kama
muhuri kwa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali, ikiwa itakuwa umeandaliwa
na kuwasilishwa bungeni bila kujumuisha ushauri wa Kamati ya Bajeti,
kama ilivyofanyika kwa ya mwaka wa fedha 2016/17.
Kuhusu suala hilo, Kamati ya Bajeti ilisema, kimsingi Serikali
kutokuwa tayari kupokea ushauri wa kamati hiyo kuhusu bajeti si sahihi
kwa sababu, wabunge kama wawakilishi wa wananchi wanahitaji kujua namna
Serikali itakavyotekeleza mahitaji ya wananchi ikiwa ni pamoja na
kutatua kero zao zinazowasilishwa na wabunge kupitia Kamati zao za
kisekta.
Akishawishi wabunge wengine kukataa kutumika kama muhuri, Mbunge wa
Mkinga (CCM), Dastan Kitandula alisema, “Wabunge tusikubali kuwa rubber
stamp (muhuri wa kuidhinisha bajeti ya serikali), ikiwa ushauri wa
Kamati ya Bajeti utakuwa umepuuzwa,” autapuuzwa.”
Post your Comment



