Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Dk John Malecela amemsihi Rais John
Magufuli kuendelea na kasi yake na kutaka asibadilike hata kama akipewa
uenyekiti wa chama hicho.
Alisema hayo wakati akizungumza kwa muda mfupi na waandishi wa habari
wakati akikabidhi madawati 127 aliyochangia na marafiki zake kwa mkuu
wa wilaya ya Chamwino, Dodoma.
Dk Malecela aliyewahi kuwa waziri mkuu na makamu wa kwanza wa Rais,
alisema kasi ya Rais Magufuli isiishie katika serikali tu, bali iingie
hadi katika chama.
“Nakubaliana na utaratibu mzima wa kumkabidhi kijiti Rais Magufuli,
lakini nataka akiingia aendeleze kasi hiyo ili amulike na kuwaondoa
wasiofaa kwenye chama”, alisema.
Baada ya kusema hayo alisema anaiunga mkono serikali ya awamu ya tano
kwa kutaka kuhakikisha kila mwanafunzi anaketi kwenye dawati na kuwaasa
walimu kuangalia utunzaji wa madawati hayo.
Post your Comment



