Wanafunzi 1,132 wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), cha Mwanza
hawatapewa matokeo yao ya kuhitimu shahada wala kushiriki katika
mahafali baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
kutolipa ada zao za mwaka huu wa masomo.
Kwa mujibu wa orodha ya
wanafunzi iliyobandikwa katika ubao wa matangazo chuoni hapo, ni
wanafunzi 933 tu watakaoshiriki katika mahafali yaliyopangwa kufanyika
Desemba 16 na 17.
Tangazo hilo lililosainiwa na Makamu wa Mkuu wa Chuo
(Taaluma), Dk Negussie Andre limewataka wanafunzi kuhakiki majina yao
kwenye orodha na kuwasilisha malalamiko au hoja zao kabla au ifikapo
Jumapili ijayo.
Kuhusu madai hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB,
Abdul Razaq Badru alisema hawezi kuyazungumzia kwa sababu kila chuo
kina mamlaka yake.
Alisema Bodi hiyo ipo kwa miaka 10 na kwamba
bila shaka kuna taasisi zinazoidai na zinalipwa kulingana na makubaliano
na mipango iliyopo akisema kila wakati kuna malipo yanayoendelea katika
vyuo mbalimbali.
Hata hivyo, alisema hana takwimu sahihi kama
na chuo hicho kimeanza kulipwa.
“Tunafanya malipo kulingana na mipango
iliyopo, kama kuna changamoto katika vyuo tunavyolipa au vinavyotudai
huwa tunajadili kwa pamoja na kupata majibu, kwa hilo lililotokea Saut
sisi kama Serikali hatuwezi kukemea wala kupongeza kwa sababu ni mamlaka
ya chuo,” alisema Badru.
Akizungumza kwa simu jana jioni, Ofisa
Mikopo wa Saut, Wilfred Medard alisema uamuzi huo umechukuliwa kutokana
na malimbikizo ya ada ya wanafunzi wanaolipiwa na bodi hiyo.
“Siwezi kutaja ghafla ni kiasi gani tunachodai, lakini kwa hakika ni zaidi ya Sh500 milioni,” alisema Medard.
Alisema
si rahisi kujua iwapo wanafunzi hao wote watashiriki mahafali kwa
sababu bado kuna fursa ya bodi kulipa madeni hayo na kuwapa nafasi ya
kushiriki mahafali na wenzao wanaojilipia au wanaolipiwa na kampuni,
taasisi na mashirika mbalimbali.
Ingawa tangazo hilo limetoa
hadi Jumapili ijayo kwa wahitimu ambao majina yao hayapo kwenye orodha
kuhakiki na kuwasilisha taarifa zao, Medard alisema bado kuna fursa ya
wahusika kukamilisha taratibu hadi Desemba 2 ambayo ni siku ya mwisho ya
maandalizi ya mahafali.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi Saut
(Sautso), Emmanuel Ayo alisema wanafunzi wanaunga mkono uamuzi wa chuo
kuishinikiza Serikali kulipa madeni hayo ili kukiwezesha kujiendesha.
“Hiki
ni chuo binafsi kinachojiendesha kupitia ada za wanafunzi. Kutolipa ada
ni kukwamisha shughuli na masomo na sisi hatuko tayari kuona tunakosa
masomo kwa sababu tu Serikali haitimizi wajibu wake wa kuwalipia
wanafunzi inaowadhamini,” alisema Ayo.
Alisema iwapo muda
uliotolewa na chuo kuhakiki utapita bila ya kulipwa kwa ada hizo, Sautso
imepanga kuonana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuwasilisha kilio chao.
“Waziri
asipotusaidia, tutakwenda hadi Ikulu kumwona Rais John Magufuli ambaye
pengine wasaidizi wake hawampi taarifa sahihi kuhusu kinachoendelea Bodi
ya Mikopo,” alisema Ayo.
Kiongozi huyo ambaye ni mwanafunzi wa
mwaka wa tatu wa shahada ya ualimu, alijitolea mfano kuwa ada yake ya
muhula wa pili mwaka jana haijalipwa hadi sasa na bodi hiyo.
Post your Comment