Mahakama Kuu Kanda ya dar es Salaam leo imemtangaza mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (Chadema) kuwa ni mbunge halali wa jimbo hilo.
Hayo yamesemwa LEO Katika Mahakama Kuu na Jaji Upendo Msuya katika hukumu ya kesi ya uchaguzi dhidi ya Mnyika iliyokuwa imefunguliwa na Hawa Ng'humbi ambaye alikuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo hilo.
Jaji huyo amesema kuwa mdai ambaye ni Nghumbi alishindwa kuthibitishia Mahakama kuhusu kesi dhidi ya Mnyika katika madai yake matano aliyokuwa aliyawasilisha mahakamani hapo na hivyo mahakama hiyo imeamuru gharama za kesi hiyo zitalipwa na Ngh'umbi.
Hata hivyo baada ya hukumu hiyo Ng'humbi alisema kuwa hawezi kusema kama ameridhika au laa kwa wakati huo.
Kwa upande wa chadema ilikuwa ni Sherehe ya ushindi,huku Mnyika akiondolewa kwa kubebwa na wana Chadema waliokuwa wamejaa mahakamani hapo ambapo Mwenyekiti wa Chama hicho,Freeman Mbowe alisema kuwa ameridhika na hukumu hiyo na kukiri kuwa mahakama imetenda haki.
Aidha mahakama hiyo imetamka kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa wa halali na kura alizopata Mnyika ni halali, Mnyika ndiye mbunge halali wa jimbo la Ubungo. Maombi ya Ng’humbi kuwa mahakama hiyo ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mnyika yametupwa mbali na Jaji Msuya.
Mahakama hiyo ilijaa wanachama wa vyama hivyo viwili ingawa wanachama wa Chadema walikuwa ni wengi zaidi hata hivyo askari walikuwa wametanda kila mahali katika mahakama hiyo pamoja na barabara ya Kivukoni kuanzia Mahakama ya Rufaa wakiwa na magari.
Baada ya Hukumu Mnyika alikumbatiana na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye alikuwepo mahakamani hapo na kutoka nje huku Mnyika akiwa amebebwa na wafuasi wa Chadema huku wakiimba kwa ushindi huo, hata hivyo hakukuwa na vurugu kubwa zilizokuwa na madhara zaidi ya maandamano yaliyoondoka mahakamani hapo wakiimba.
Mbowe aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kesi hiyo imetumia zaidi ya Sh bilioni mmoja hivyo kesi kabla ya kusikilizwa ichunguzwe zaidi ikionekana haina hoja za msingi ni vizuri kutupwa mapema. Hata hivyo alisema “ mahakama imetenda haki na hii inaonyesha namna ambavyo inaweza kutenda haki hata katika vyama vya upinzani.”
Kwa upande wake Hawa Ng’humbi alisema kuwa amepokea maamuzi yaliyotolewa na Mahakama lakini hawezi kusema lolote kwa wakati huo na kwamba wana CCM wawe na utulivu kwasababu anaamini ni watulivu kama kuna jambo tofauti atazungumza baadaye.
Hukumu hiyo imesomwa leo katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kwa takribani saa moja na nusu kuanzia saa 4 asubuhi na Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Jaji Upendo Msuya ambaye aliamuru kuwa gharama za kesi hiyo zitabebwa na mdai (Hawa Ng’umbi).
Jaji Msuya katika hukumu hiyo alisema kuwa Ng’humbi katika madai yake yote matano hakuna hata moja alilolithibitisha kama ambavyo sheria inamtaka mdai katika kesi ya uchaguzi, kuthibitisha dai lake bila kuacha shaka yoyote na pia kutoa ushahidi kuonyesha ni namna gani iliathiri matokeo ya uchaguzi.
Katika hukumu hiyo, jaji huyo alisema kuwa Ng’humbi na mashahidi wake aliowawasilisha mahakamani hapo hawakuonyesha wala kuthibitisha madai yaliyowasilishwa mahakamani kwamba yalitendeka, na pia iliathiri matokeo ya uchaguzi uliofanyika Octoba 31,2010.
“Nilipata nafasi ya kupitia ushahidi wa kila shahidi pamoja na vielelezo vilivyotolewa mahakamani katika kesi hii lakini nimeshangaa ni kwanini mdai hakuleta mahakamani mashahidi ambao walikuwepo katika chumba cha majumuisho ya kura ambako ndiko madai hayo yalikotokea,” alisema jaji Msuya.
Alisema hata hivyo hakuelewa ni kwanini watu zaidi hawakuletwa kuunganisha ushahidi wao kuthibitisha madai ya mdai na pia kama kweli madai hayo yalitokea ni kwanini wagombea wengine au watu waliokuwa katika chumba cha majumuisho hawakulalamika.
Fomu namba 24 b ilikuwa na dosari na ndiyo ilikuwa inabishaniwa na Ng’humbi ilikosewa kuandika. Kura halali ni Mnyika aliyetangazwa kuwa ni mshindi alipata kura 66,742 wakati Ng’humbi kura 50,544. Wagombea wote kura 132496.
Alisema kuwa katika ushahidi wa mdai hakuonyesha ni vipi ongezeko hilo la kura liliathiri matokeo ya uchaguzi na pia mdaiwa Mnyika anahusika vipi na ongezeko hilo.
Hata hivyo jaji huyo kabla hajaanza kuchambua hoja za Ng’humbi aliwapongeza mawakili katika kesi hiyo ambao walijitahidi kuwasilisha mashahidi na kuhoji maswali ya msingi bila kupoteza muda kwa kuuliza maswali yasiyo na msingi na pia kuwasilisha pingamizi zinazopelekea shauri kuwa na mlolongo mrefu.
Dai la udhalilishwaji na kuitwa fisadi na Mnyika katika mkutano alioufanya kwenye kampeni ambapo alidai kuwa Ng’humbi aliuza nyumba ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT), na kwamba watu wasichague CCM inakumbatia mafisadi.
Jaji Msuya alisema madai hayo kwa mujibu wa ushahidi wa mdai maneno hayo yaliongewa na Mnyika kwenye mkutano ambao ulikuwa na watu zaidi ya 500 lakini yeye hakuwepo hivyo mahakama haichukui maneno ya kuambiwa bali mtu aliyesikia mwenyewe au kushuhudia.
“hata hivyo katika watu wote hao 500 waliokuwa kwenye mkutano hakuja hata mtu mmoja kutoa ushahidi, na pia haikuthibitishwa ni namna gani iliathiri uchaguzi na hivyo hoja hiyo imeondolewa,” alisema Jaji Msuya.
Dai la Mnyika aliingia na wafuasi wengine wa CHADEMA kwenye kujumlisha matokeo, jaji huyo alisema kuwa ushahidi pekee ni wa mdai na kwamba hadhani kuwa ni jambo linalowezekana mtu asiyehusika kuingia katika chumba cha majumuisho ya kura wakati kulikuwa na ulinzi na kwamba wagombea wengine wangelalamikia jambo hilo hata hivyo mdai hakuleta mashahidi waliokuwa katika chumba hicho kutoa ushahidi kuwa kuna watu wasiohusika waliingia.
Aidha dai la msimamizi wa uchaguzi alitumia kompyuta ndogo (laptop) za Mnyika badala ya rasmi za tume ya uchaguzi na pia hazikukaguliwa na kwamba pengine kulikuwa na taarifa zisizo rasmi kwenye kompyuta hizo ikiwa ni pamoja na ongezeko lile la kura 14,000.
Jaji Msuya alisema kuwa kwa mujibu wa ushahidi hazikutumika kompyuta za mnyika na kwamba zilikuwa za mawakala na kwamba katika hili Mdai angeweza kuleta mashahidi zaidi kuthibitisha ikiwa ni pamoja na mkurugenzi wa uchaguzi.
Post your Comment