Ni katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi WAKUU wa nchi za Afrika wametaka
kuwepo na juhudi za pamoja katika kukabiliana na majanga yatokanayo na
mabadiliko ya tabiachi yanayolikumba bara hilo.
Kauli hiyo ilitolewa jana mchana
(Jumanne, Mei 24, 2016) wakati wa majadiliano baina ya viongozi kutoka
Zambia, Chad, Nigeria, Msumbiji na Tanzania mara baada ya ufunguzi wa
Mkutano wa 51 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano cha kimataifa wa Mulungushi,
jijini Lusaka, Zambia.
Wakishiriki kwenye mjadala wa
Wakuu wa Nchi na Serikali uliohusu Nishati na Mabadiliko ya Tabianchi,
viongozi hao walisema bara la Afrika linahitaji kupata maendeleo zaidi
licha ya tatizo la nishati linalolikumba bara hilo hivi sasa.
Akichangia mjadala huo, Rais wa
Zambia, Bw. Edgar Lungu alisema nchi yake imepania kuboresha hali ya
upatikanaji wa umeme vijijini lakini imekuwa ikikabiliwa na tatizo la
uhaba wa mvua kwa zaidi ya miaka miwili hali ambayo alisema imechangia
kukosekana kwa umeme katika maeneo mengi nchini humo.
“Uhaba wa mvua umepunguza kiwango
cha maji katika bwawa la Kariba ambalo hutumika kuzalisha umeme nchini
mwetu. Na hapa kwetu, karibu asilimia 80 ya umeme wetu, unategemea
uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vya maji,” alisema.
Rais wa Chad, Bw. Idriss Deby
Itno aliitaka benki ya AfDB ichukue nafasi ya mdau mkuu kwenye uwekezaji
wa sekta ya nishati na kuzisadia nchi za bara hili kupata mitaji ya
uwekezaji na ushauri wa kitaalamu.
“Tunahitaji kutumia fursa ambazo
benki yetu inazo katika kukabilianana changamato za ukosefu wa nishati.
Tukiweza kutekeleza jambo hilo, tutafanikiwa kuwa na miradi ambayo ni
makini na kwa maana hiyo tutaweza kuliangaza bara letu la Afrika kwa
kupata mwanga wa uhakika,” alisema.
Kwa upande wake, Makamiu wa Rais
wa Nigeria, Prof, Yemi Osinbajo alisema bara la Afrika halina budi budi
kuweka kipaumbele kwenye masuala ya maendeleo yake wakati likitafuta
suluhisho la kukabiliana na athari za mazingira.
“Tunapaswa kutafuta njia za kubalance
mahitaji makubwa ya umeme ambayo bara letu linakabiliwa nayo dhidi ya
athari za kimazingira ambazo zinapigiwa kelele na mataifa makuna na
zinahatarisha kutunyima fursa ya kuendelea haraka kama ilivyokuwa kwao,”
alisema na kuongeza:
“Kama nchi zilizoendelea zinataka
sana kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, zinatakiwa
zitupatie fedha, teknolojia na wataalamu ambao watasaidia kuendesha
mitambo ili tupate nishati safi kutokana na mafuta ya petroli na dizeli
sababu ni rasilmali ambazo tunazo.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
alisema ili kuondokana na tatizo la nishati, kuna haja ya kuwa na
viongozi wenye utashi wa kisiasa ambao watakuwa tayari kuruhusu
uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya nishati na kuongeza kuwa Tanzania
inapitia upya sheria zake ili kuruhusu miradi mikubwa ya uwekezaji
kwenye sekta hiyo.
Aliwaambia washiriki wa mkutano
huo kwamba milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi kwa ajili ya
wawekezaji walio tayari kuwekeza kwenye sekta hiyo na kutaja fursa
ambazo Tanzania inazo kwenye sekta ya nishati ikiwemo gesi asilia, makaa
ya mawe, madini ya urani, maji, upepo na nishati ya joto kutoka ardhini
(geothermal energy).
Naye Waziri Mkuu wa Msumbiji, Bw.
Carlos Agostinho do Rosário alisema kuna haja ya kuwa na taasisi ya
uzalishaji na ugawaji umeme ya pamoja (electricity pool) ambayo
itaruhusu wazalishaji wa umeme wawauzie wanunuzi wakubwa.
Waziri Mkuu ambaye yuko Lusaka
kuhudhuria mkutano huo wa ADB kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John
Pombe Magufuli, amerejea nchini leo (Jumatano, Mei 25, 2016).
Post your Comment



