WABUNGE bila kujali tofauti zao za kiitikadi, wamelalamikia mitaala
mibovu inayotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, ikiwemo kila waziri kufika na mfumo wake. Pia wamelalamikia
mitaala kukosewa na kutaka Rais John Magufuli kuifumua wizara hiyo na
kuiunda upya.
Wakichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya wizara hiyo juzi jioni
bungeni, wabunge hao walionesha kukerwa na jinsi wizara isivyo na mtaala
wa aina moja. Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alisema
Waziri akiingia katika wizara ndiyo mfumo, huku akimtaja Waziri
aliyepita, Dk Shukuru Kawamba, kwamba aliyoyafanya yamepinduliwa yote na
Waziri Ndalichako ambaye alidai akiondoka, atakayekuja atayapindua
yote.
“Hii inatia tatizo sana, hivi mambo ya BRN (matokeo makubwa sasa )
yameenda wapi?” Alihoji? Alisema Sera ya Vitabu ya Mwaka 1991, iliruhusu
sekta binafsi waandike vitabu na taasisi ya elimu wakague vitabu na
kuhoji ni nani anahariri vitabu leo hii, huku akidai kuwa magazeti
yanahaririwa vizuri siku hizi kuliko vitabu vya shule.
Mbatia alisema Sera ya Elimu iliyozinduliwa mwaka jana imetumia zaidi
ya Sh bilioni 50, lakini katika ukurasa wa 22 inaelezwa kuwa mtaala
unafundishwa, huku ukurasa wa 27 ukisema mtaala ni mwongozo mpana.
Alisema kuna kitabu kimeandikwa mbili mara saba kinasema 15, kitabu cha
hisabati darasa la kwanza pale mwanzoni kinasema namba nzima ni 1 hadi
99, ukiangalia cha Kiingereza Chapter 4 inaanza na aeiou wakati mwanzoni
ndiyo wanaanza na sentensi ni vitu vya ajabu sana.
“Elimu ndiyo mapigo ya moyo ya taifa, mapigo hayo ya moyo yakizimika
taifa nalo limezimika. Hivyo namwomba Rais Magufuli afumue wizara yote
ya elimu kwani kuna ufisadi wa kutisha hasa taasisi ya elimu ndiyo hovyo
kabisa,” alisisitiza. Mbunge wa Mwibala, Kangi Lugola (CCM) alisema
kila waziri anakuja na mfumo wake kwa kuanzisha mitaala yake kwa kufumua
ya mwenzake aliyetangulia.
“Waziri lazima hili kuliangalia haiwezekani kila waziri anayekuja
kuwa na mfumo wake kwa kufumua ya wengine, jambo linalofanya kusiwe na
mfumo mmoja wa mtaala,”alisema. Naye mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda
Hassan (CHADEMA) alisema mitaala iliyopo sasa haiendani na soko la ajira
nchini na hata katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na inawaacha
watoto masikini katika ombwe kubwa.
Naye Mbunge wa Maswa, Mashimba Ndaki (CCM) alisema baada ya kuweza
elimu bure, kulikuwa na suala la kujenga maabara ambalo limetoweka na
kuanza ununuzi wa madawati. Huku akishangaa suala la ununuzi wa madawati
yanakaa wapi wakati shule nyingi hazina majengo ya kutosha. Naye,Mbunge
wa Viti Maalumu, Ester Mahawe (CCM) alisema kwa sasa nchini hakuna
mfumo maalum wa mitaala ya kufundishia kutokana na kubadilishwa kila
wakati bila kuwa na tija.
Alisema hatua hiyo inatokana na kila waziri kuja na masuala yake
kwani zamani kulikuwa ma mfumo mmoja nchi nzima, hivyo ni vema
kuangaliwa ni wapi wizara hiyo ilianguka na kusimama kisha kuendelea
kuboresha elimu.
“Nakumbuka miaka ya nyuma kulikuwa na mashairi tunaimba wanafunzi wa
nchi nzima kama ile ya ‘Karudi baba mmoja toka safari ya mbali kavimba
miguu,kutokana na kuwa na mtaala mmoja,’” alisema.
Naye Mbunge wa Bihalamulo Magharibi (CCM), Oscar Mukasa alisema suala
la mitaala limekuwa tatizo nchini hasa baada ya walibadilisha mitaala
hivi karibuni ya darasa la kwanza na la pili na kuleta KKK yaani
kuandika, kuhesabu na kusoma na sasa walimu wanabahatisha tu. Alisema
hatua hiyo inatokana na kuwa awali walikuwa na mtaala mwingine ambao
kabla haujaonesha mafanikio yeyote umeondolewa hivyo wanafunzi wanabaki
wakibabaika.
Mbunge huyo alikuwa na vitabu vitatu vya Sayansi viwili vya darasa la
sita na kimoja darasa la saba, lakini kila kimoja kikieleza aina za
ubongo tofauti. Alisema kimoja cha darasa la sita kinaeleza ubongo una
sehemu tatu na kile cha darasa la saba ubongo una sehemu nne na kutaka
vitengo vya ukaguzi kuimarishwa ili kujua wanafunzi wanafundishwa nini.
Mbunge Asunga, alisema ni vema wizara hiyo kuangalia mitaala kwani ya
sasa haiwafanyi vijana kujitegemea kwa kutoendana na vipaumbele vya
nchi kuendana na soko la ajira. Naye, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Maftah
Nachuma (CUF) alisema suala la elimu limekuwa likiwekwa danadana kwa
kila waziri anayeingia na kuja na mitaala yake kwa kubadilisha mfumo wa
elimu.
“Kila waziri anayekuja na kutunga sera za elimu mwisho wa siku,taifa
hatuna sera wala mitaala mmoja tunabaki tunayumba yumba na hatuwezi
kufikia malengo ya Mwalimu Nyerere kuweza kujikomboa mwenyewe wala jamii
inayomzunguka,” alisema.
Alisema hawezi kujikomboa kwa kuwa elimu anayopata kwa kuwa haina
dira wala muelekeo inakuwa si elimu bora, kwa kuwa kuna wizara mbili ya
Tamisemi na Elimu zinashughulikia elimu. Alisema yeye akiwa mkuu wa
shule kwa miaka 12 hajui tofauti ya vitu vinavyoshughulikiwa na Wizara
ya Tamisemi na Wizara ya Elimu na kuona kitu kimoja.
Naye Mbunge wa Mbozi, Pascal Ahonga (CHADEMA) alisema suala la
mitaala kila mtu anapanga ya kwake kila waziri anachanganya kutokana na
ukosefu wa viongozi bora.
Post your Comment



