SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema uchunguzi unaendelea
kuwabaini watu waliohusika na kuvuruga uchaguzi wa Oktoba 25 na
kusababisha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuitisha uchaguzi mwingine wa
marudio.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mohamed Aboud Mohamed wakati akijibu swali la mwakilishi wa jimbo la
Fuoni, Yussuf Hassan Iddi aliyetaka kufahamu waliovuruga uchaguzi wa
Oktoba 25 wamechukuliwa hatua gani hadi sasa.
Alisema uchunguzi wa kina unahitajika kwa sasa ikiwemo kukusanya
vielelezo kutoka kwa watu mbalimbali, ikiwemo watendaji wa Tume ya
uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi ambao waliohusika na matukio hayo.
Alikiri na kusema suala hilo limechukua muda mrefu takriban miezi
saba tangu uchaguzi huo kufutwa na kufafanua kuwa kufungua mashtaka
kunahitajika uchunguzi wa kina. “Mheshimiwa Spika napenda kusema kwamba
Serikali ipo katika hatua za uchunguzi wa tukio hilo ambalo linahitaji
muda mrefu wa kufuatilia wale wote waliohusika,” alisema.
Aboud alisema mara baada ya uchaguzi wa Oktoba kuvurugika, serikali
ilifanya wajibu wake kwa kuipatia fedha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
(ZEC) na kuiwezesha kufanya uchaguzi mwingine.
Alisema uchaguzi wa marudio ulifanyika katika mazingira ya amani na
utulivu na viongozi kuchaguliwa na kushika hatamu ya kuongoza
nchi.Aliwaeleza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa serikali
haijalifumbia macho suala hilo kwa sababu imetumia fedha nyingi za
dharura kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi wa marudio unafanyika.
“Serikali kamwe haijalifumbia macho suala la watendaji waliovuruga
uchaguzi wa marudio na kupelekea kuitia hasara serikali...suala hilo
lipo katika mikono ya vyombo vya uchunguzi na upelelezi kwa hatua
nyingine,” alisema.
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilifuta uchaguzi wa Oktoba 25
mwaka jana kwa madai ya kujitokeza kwa kasoro mbalimbali ambazo
zilionesha kwamba uchaguzi huo usingekuwa huru na haki na kuibua
malalamiko pande zote.
Post your Comment



