Serikali
ya Tanzania imepitisha bajeti ya shilingi trilion 29.5 kwa kupigiwa
kura huku wabunge wa upinzani wakiwa wametoka nje wakiwa wameziba midomo
yao kwa karatasi na plasta ikiwa ni ishara ya kuonesha kutoridhika na
Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson wakigomea vikao vya Bunge vinavyoongozwa
na Naibu Spika huyo
Katika vikao vya Bunge la 11, wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa
wakisusia vikao hivyo kwa takribani siku 23 sasa kwa madai ya
kutokubaliana na ukandamizaji unaofanywa na Naibu Spika wa Bunge
Dkt.Ackson Tulia.
Wakichangia bajeti hiyo, Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter
Mwijarubi Muhongo pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Charles
Mwijage wamesema bajeti hiyo inalenga kukuza uzalishaji.
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia katika Bajeti hiyo
ikiwa ni pamoja na ya kuongeza fedha katika ofisi ya mkaguzi wa serikali
CAG ili kutanua wigo wa ukaguzi pamoja na kuachana na mpamgo wa kuanza
kuwakata kodi wabunge katika mafao ya kiinua mgongo ya Wabunge, Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Phillip Mpango amesema msimamo wa serikali upo
pale pale.
Kuhusiana na makato ya kodi kwenye mafao ya wabunge, Dkt Mpango
amesema kuwa serikali imeamua kuwa itakata kodi hiyo kwa viongozi wote
wa kisiasa wakiwemo wakuu wa wilaya, wakuu wa mkoa, Waziri Mkuu, Makamu
wa Rais na Rais pia, ili kuweka usawa katika makato ya kodi nchini.
Baadaye jioni wabunge walipiga kura mmoja mmoja kupitisha bajeti
hiyo, ambapo wabunge wote 251 waliokuwemo bungeni walipitisha bajeti
hiyo kwa kauli moja, ambapo kila mbunge alijibu "Ndiyo" akimaanisha
anaipitisha bajeti hiyo.
Akitangaza matokeo ya kura baada ya wabunge kuipigia kura Bajeti hiyo
Bungeni, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah amesema Idadi ya
wabunge wote waliokuwepo ukumbini ilikuwa 252 ambapo kati yao waliopiga
kura za ndiyo walikuwa 251 huku kukiwa hakuna kura ya hapana.
Aidha, kura moja ambayo haikupigwa ilikuwa kura ya Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson ambayo kwa kawaida huwa ni kura ya maamuzi.
Dk. Kashilillah amesema idadi ya wabunge wote Kikatiba ni 393 lakini
hadi sasa wabunge waliopo ni 389 huku wabunge 137 walikuwa hawapo
ukumbini.
Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Naibu Spika
amesema Bajeti hiyo imepitishwa kwa kishindo kwa kuwa kwa mujibu wa
Kanuni za Bunge, akidi ya kikao cha Bunge kuendelea ni nusu ya wabunge
ambao ni 195 na ili Bajeti hiyo ipitishwe ilitakiwa kupigiwa kura ya
ndiyo na nusu ya akidi ya wabunge 195 ambao ni wabunge 98.
Upitishwaji wa Bajeti hiyo ni umefanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 107
(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge ambayo inaelekeza kwamba mjadala kuhusu
Hotuba ya Bajeti utakapomalizika huku Kanuni ya 77 (1) ikieleza idadi
ya wabunge wakati wa kufanya maamuzi kwamba itakuwa ni nusu ya wabunge
wote.
Wakati huohuo Bunge limepitia Muswada wa Sheria ya kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa mwaka 2016.Muswada huo umepitishwa leo katika hatua zake zote mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Serikali.
Akielezea namna ya upitishwaji wa Muswada huo, Naibu Spika, Dk. Tulia
Ackson amesema ni tofauti na miswada mingine kwa kuwa hautangazwi
katika Gazeti la Serikali na wala haujadiliwi na wabunge.
Mapema Asubuhi mara baada ya dua, wabunge wa upinzani waliziba midomo
yao kwa karatasi na Plasta na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge ikiwa ni
ishara ya kuonesha kutoridhika na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia
Ackson.
Mbunge wa Vunjo Kupitia chama cha NCCR Mageuzi, Mhe. James Mbatia kwa
niaba ya wabunge hao amesema hawataacha kulalamikia ukiukwaji wa sheria
unaofanywa na kiti cha Naibu Spika.
Baadhi ya wabunge wa Vyama vya Upinzani wamekuwa wakisusia vikao hivyo Tangu Mei 30 mwaka huu.
Post your Comment



