KATIBU
wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah leo ataeleza kinachoendelea kuhusu
kusudio la Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutaka kumwondoa madarakani
Naibu Spika, Dk Tulia Ackson (pichani).
Kambi
hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Taifa, Freeman Mbowe katika migomo yake dhidi ya vikao
vinavyoongozwa na Dk Ackson, iliwasilisha kusudio hilo kwa Ofisi ya
Spika wa Bunge wiki iliyopita kwa maelezo kuwa haina imani naye.
Kwa
mujibu wa Dk Kashillilah, ataeleza kinachoendelea leo baada ya kumaliza
kupitia taratibu zote na kujiridhisha kuhusu kila hatua inayopaswa
kufuatwa kuhusu suala la aina hiyo.
“Nitaeleza kinachoendelea kesho (leo) baada ya kujiridhisha kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa kuhusu suala hilo,” alisema.
Katika
kusudio hilo lililowasilishwa na Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya,
Kambi hiyo ya Upinzani ilieleza mambo sita yaliyoisukuma kuona kuwa Dk
Tulia hafai kuendelea kushika kiti cha Naibu Spika.
Mambo
hayo ni upendeleo kwa wabunge wa CCM, kusimamia maslahi ya Serikali
badala ya umma, kutokuwa mwanasiasa, jambo linalomfanya akose uzoefu wa
kuendesha vikao vya Bunge, ubabe, unyanyasaji kwa wabunge wa upinzani na
kusimamia fedha za Mfuko wa Bunge zirudishwe kwa Rais.
Millya
alisema walipeleka kusudio hilo kwa Ofisi ya Spika kwa kuzingatia ibara
ya 85(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozungumzia
hatua za kuchukua ili kumwondoa madarakani Naibu Spika.
Ibara
hiyo inasema, “Naibu Spika atakoma kuwa Naibu Spika na ataacha kiti cha
Naibu Spika ikiwa mtu huyo ataondolewa kwenye madaraka ya Naibu Spika
kwa azimio la Bunge.
Hata
hivyo, inaelezwa kuwa ili hoja hiyo ijadiliwe bungeni italazimika
kujadiliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya
Bunge ambayo nayo inahitaji theluthi moja ya saini za wabunge wote.
Post your Comment



