CHAMA Cha Kijamii (CCK) kimelaani mpango unaofanywa na wabunge wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wa kutaka kumng’oa Naibu Spika wa
Bunge, Dk Tulia Ackson na kimewataka kufuata kanuni za uendeshaji wa
Bunge.
Hayo yamo kwenye taarifa ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCK, Constantine
Akitanda aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, iliyotokana na tathmini
ya Bunge tangu kurejeshwa Mfumo wa vyama vingi vya siasa, chanzo na
kupevuka kwa ususaji wa shughuli za Bunge.
Kuhusu mpango wa kutaka kumng’oa Dk Tulia, Mwenyekiti huyo wa CCK
alisema; “Hivi sasa kuna propaganda inayoenezwa ya kutaka kumng’oa Naibu
Spika, Dk Tulia Ackson kwa madai ametumwa na Rais kuminya uhuru na
demokrasia ndani ya Bunge.
“Hii si mara ya kwanza kwa kambi ya rasmi ya upinzani kulalamikia
kiti cha Spika. Pia si mara ya kwanza kwa kambi hiyo kususa na kutoka
nje ya bunge, pia si mara ya kwanza wabunge wa upinzani kukorofishana na
kiti cha spika na kususa,” alisema.
Akitanda alisema tatizo la kambi hiyo ni pale spika anaposimamia
kanuni huku wao wakikataa kwa makusudi, kufuata taratibu na kanuni za
uendeshaji wa shughuli za Bunge, jambo alilosema haliwezi kufumbiwa
macho.
“Kanuni zipo wazi kama hujaridhika na maamuzi ya kiti cha Spika
unaruhusiwa kukata rufaa na hoja ikajadiliwa, sasa wabunge wetu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani sijui ni kwa nini hawataki kufuata utaratibu huu,
ambao ni wa kikanuni.Wao wanataka kumng’oa Naibu Spika tu basi, kanuni je?”
Alisema dalili za kukataliwa kwa Naibu Spika na wabunge hao zilionekana tangu mwanzo kwani walimkataa hata kabla ya kuanza kazi kwa madai kuwa ametumwa na Ikulu, na hata siku ya kujieleza akiomba kura alikuwa anazomewa na wabunge wa kambi hiyo.
Alisema dalili za kukataliwa kwa Naibu Spika na wabunge hao zilionekana tangu mwanzo kwani walimkataa hata kabla ya kuanza kazi kwa madai kuwa ametumwa na Ikulu, na hata siku ya kujieleza akiomba kura alikuwa anazomewa na wabunge wa kambi hiyo.
“Kimsingi tangu mwanzo wabunge wetu wa upinzani hawakumtaka Dk Tulia
kutokana na umahiri wake wa kuzijua na kuzisimamia kanuni kwa ustadi
mkubwa.” Akitanda alisema tangu Bunge la vyama vingi lianze mwaka 1995,
wabunge wa upinzani kutokana na uchache wao wamekuwa wanalalamikia kiti
cha Spika na kutofautiana na Spika au kudai wanaburuzwa na wenzao wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi sasa ambapo Chadema kwa
mara ya pili imetoa kiongozi wa upinzani bungeni, nchi imeshuhudia
wabunge wa upinzani wakitumia muda mwingi kulalamikia kiti cha Spika.
“Kwa kipindi cha 2010 hadi 2015, Spika wa Bunge alikuwa Anne Makinda
na Naibu Spika Job Ndugai. Wapinzani walimlalamikia sana spika
wakimtuhumu kuwa anailinda serikali na kuwa kiti cha Spika kimemshinda.
Alisema picha ambayo Watanzania wanaipata kutoka kwa Kambi Rasmi ya
Upinzani yenye nia ya kumng’oa Dk Tulia kwa kupiga kura ya kutokuwa na
imani naye, ni mwendelezo wa wazi wa udhalilishaji wa wanawake kuwa
hawana uwezo wa kuongoza.
Post your Comment



