POLISI imepiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara, iliyokuwa
imepangwa kufanywa na baadhi ya vyama vya siasa. Kwa mujibu wa Kamishna
wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, siku za hivi karibuni
jeshi hilo limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa,
vikitaka kufanya mikutano na maandamano, lakini wamepiga marufuku
maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia jana hadi hapo hali ya usalama
itakapotengemaa.
Bila kutaja vyama vilivyowasilisha maombi, taarifa hiyo imesema
polisi kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya habari, limebaini kuwa
mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za
nchi.
“Aidha vyama vingine vya siasa vimeonesha dhamira ya kupinga kile
ambacho kitasemwa na wapinzani wao,” alisema Mssanzya katika taarifa
yake bila kufafanua vyama husika. Ingawa hakufafanua vyama
vitakavyopinga kile kitakachosemwa na wapinzani wao, taarifa hiyo
inatafsiriwa kuwa kulitegemewa kuwapo mikutano ya chama tawala na vya
upinzani.
Taarifa hiyo ya Mssanzya iliendelea kusema kwamba vyanzo hivyo vya
habari, vimebainisha kwamba upo uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu baina
ya makundi mawili ya kisiasa. Aliwataka wanasiasa kuacha mara moja
kushinikiza wananchi kutotii sheria za nchi. Alisema hawatasita
kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote au chama chochote cha
siasa, kitakachokaidi agizo hili.
Aidha, jeshi hilo limewataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wenye
lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi. Mssanzya aliwasihi wananchi
waendelee kushirikiana katika kujenga umoja wa nchi.ACT yalia na polisi
Wakati huo huo, Chama cha ACT Wazalendo kimelaumu uamuzi huo wa
polisi wa kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Chama hicho
kilisema uamuzi huo wa polisi, unatokana na kuzinduliwa kwa mpango wao
wa ‘Operesheni Linda Demokrasia’ kumpa fursa Mbunge wa Kigoma Mjini,
Kabwe Zitto na wabunge wengine wa upinzani, waliosimamishwa bungeni
kuwaeleza wananchi juu ya kile kinachodaiwa ni kuminywa kwa demokrasia
bungeni.
“Mikutano ya ‘Operesheni Linda Demokrasia’ inayoratibiwa na chama
chetu ilipangwa kufanyika kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma,
Katavi, Rukwa, Mbeya na Morogoro, mpaka sasa umeshafanyika mkutano
mmoja jijini Dar es Salaam,” ilisema taarifa ya Katibu Itikadi,
Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu.
Chama hicho kilituhumu Jeshi la Polisi kuwa limeminya haki ya
kisheria ya vyama kufanya mikutano. Kimesema kinawasiliana na wanasheria
wake kupata tafsiri ya kimahakama ya uhalali wa polisi kuzuia mikutano
ya vyama vya siasa ambayo inatambuliwa na kulindwa na katiba.
CCM ilishajiandaa
Amri hiyo ya polisi imekuja siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kupitia kwa msemaji wake, Christopher Ole Sendeka kukaririwa na
waandishi wa habari, akishutumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Alisema chama hicho cha upinzani, kinataka kwenda kuishitaki serikali
kwa wananchi kwa hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa kuziba mianya ya
rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.
Sendeka alisema atahakikisha kila watakapotoka (vyama vingine)
kufanya mikutano yao, ataingia na Watanzania watapima kati ya kauli ya
wanaowakilisha mafisadi wanaokwepa kodi, watumishi wavivu na watendaji
wanaohakikisha kodi ya Watanzania inatumika vizuri.
“Kama hoja zao ni hizi nawaonea huruma sana, wanafikiri kama
Watanzania watawaunga mkono, nina hakika si tu kwamba hawatawaunga
mkono, bali Watanzania wataendelea kuwashangaa na chati yao itashuka,”
alisema.
Sendeka alisema ni jambo la ajabu kuona wakati serikali inashughulika
na walanguzi wachache, ambao wamekuwa wakilikosesha taifa mapato,
kikundi cha watu wachache wanakwenda kukisemea kikundi hicho na kuitaja
Tanzania kama nchi ya kifashisti na kidikteta jambo ambalo si sawa.
Mabomu yatawanya Chadema
Wilayani Kahama, Polisi kwa kushirikiana na wa Mkoa wa Shinyanga,
jana waliwasambaratisha kwa kutumia mabomu ya machozi na gari la maji ya
kuwasha wafuasi na viongozi wa juu wa Chadema, waliokuwa wakitaka
kufanya mkutano mjini hapa kinyume cha sheria.
Tukio hilo lilitokea saa 7 mchana kwenye viwanja vya CDT wakati
viongozi hao wa ngazi za juu wa chama hicho, walipokuwa wakitaka kufanya
mkutano wa kufungua kampeni ya “Operesheni Okoa Demokrasia Kanda ya
Ziwa. Katika tukio hilo, viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti
wa Taifa, Freeman Mbowe, magari yao yalimwagia maji hayo ya kuwasha
baada ya kuingia katika viwanja hivyo kuanza mkutano wao huo.
Hata hivyo, baada ya kutokea hali hiyo ya sintofahamu, wananchi
walikimbia ovyo kukimbia mabomu ya machozi yaliyokuwa yakipigwa na
askari wa Jeshi la Polisi Kahama kwa kushirikiana na wale waliopo mjini
Shinyanga, waliokuja kwa ajili ya kuongeza nguvu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Mbowe alisema
kitendo walichofanyiwa na Polisi, sio cha kiungwana na kuwa taarifa za
kufanya mkutano waliokuwa nazo tangu juzi, hivyo haiwezekani kuwazuia
jana.
Mbowe alisema hawataacha kufanya mikutano yao hiyo, akidai haki ya
kila mwananchi kupata taarifa na kwamba kwa sasa wanakaa vikao vya
ndani, kujadili suala hilo na ikibidi watalifikisha mahakamani kwa fujo
walizofanyiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange alisema walisitisha
mkutano huo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo zile za
kiintelejensia, walizokuwa nazo kuhusu mkutano huo.
Post your Comment



