SERIKALI inajiandaa kutumia Sh bilioni moja katika ujenzi wa kila
jengo moja la Kamanda wa Polisi ili kukidhi mahitaji ya majengo 15 ya
makamanda hao nchi nzima. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad
Yusufu Masauni alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa
Igalula, Musa Ntimizi (CCM).
Ntimizi katika swali lake, alisema mazingira ya makazi ya polisi
katika Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Uyui, Isikizya ni magumu kwa sasa
ambapo askari wanaishi katika nyumba za kupanga na katika mabanda ya
mabati, yaliyojengwa karibu na kituo.
Kutokana na hali hiyo, alitaka serikali ieleze ina mpango gani wa
kuboresha mazingira hayo kwa askari wetu, ili wafanye kazi katika
mazingira bora zaidi. Akijibu swali hilo, Masauni alisema ujenzi wa
vituo vya Polisi, majengo ya utawala na nyumba za kuishi askari, ni
suala linalohitaji fedha nyingi kwa nchi nzima.
Alisema kwa sasa kuna upungufu katika vituo vya Polisi daraja A na
Daraja B, ambavyo ni vituo vinavyotakiwa kujengwa katika makao makuu ya
wilaya na mikoa ya kipolisi na katika miji inayokua.
Kwa mujibu wa Masauni, vituo vya daraja A vinavyotakiwa kujengwa nchi
nzima ni 94, kwa wastani wa Sh bilioni 94 na vituo daraja B
vinahitajika 382, kwa gharama ya Sh bilioni 191 na vituo Daraja C
vinavyohitajika 4,043 kwa gharama ya Sh bilioni 950.
Mbali na vituo hivyo, Masauni alisema pia kuna mahitaji ya nyumba za
kuishi askari 35,000 ambazo ujenzi wake umekadiriwa kutumia Sh trilioni
2.8. Kutokana na hali hiyo, Masauni alisema kila mwaka Serikali ina
mpango wa kujenga nyumba 3,500 nchi nzima.
Pia alisema Serikali ya Awamu ya Tano, ina mpango wa kujenga nyumba
nyingine 4,136 kutokana na mkopo wa dola za Marekani milioni 500 kutoka
nchini China na tayari mpango huo upo Wizara ya Fedha na Mipango.
Kuhusu ujenzi wa vituo vya Polisi Daraja A, B na C na majengo ya
makamanda, Serikali itaendelea kujenga kulingana na uwezo wa upatikanaji
fedha. Alisema pia wizara yake, itaendelea kuwasiliana na serikali za
mitaa, ili panapoanzishwa wilaya na mikoa, kuwepo na huduma zinazohusu
ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya Polisi na nyumba
za kuishi askari.
Post your Comment


