WAKATI leo Waislamu kote nchini wanaanza mfungo wa mwezi mtukufu wa
Ramadhani, wafanyabiashara katika baadhi ya masoko jijini Dar es Salaam
wamesema kuwa bidhaa zinazotumiwa kwenye mwezi huo baadhi zimepanda bei
Katika Soko la Kariakoo, bidhaa za ndizi, viazi na magimbi zimepanda
huku kwenye masoko ya Ilala na Buguruni bidhaa hizo bei zake zikiwa
hazijapanda kwa kile kilichoelezwa kuwa bidhaa nyingi ndio msimu wake.
Mfanyabiashara
wa Soko la Kariakoo, Ashura Juma alisema bei hizo zimepanda kwani mkungu
mmoja wa ndizi kwa sasa unauzwa kuanzia Sh 20,000 hadi 50,000 wakati
awali walikuwa wananunua Sh 20,000 hadi 40,000.
Juma alisema kutokana na kupanda kwa bei hizo, wanalazimika na wao
kupandisha bei na kwamba ndizi tatu wanauza kwa Sh 1,000. Pia alisema
mazao ya magimbi hununua kwa gunia Sh 80,000 wakati awali walikuwa
wananunua kwa Sh 50,000.
Mfanyabiashara katika Soko la Ilala Boma, Mussa Hassan alisema bei za
vyakula hazijapanda kwa kuwa bidhaa nyingi ndio msimu wake. Alisema bei
hizo zinaweza kupanda kuanzia leo na siku zinazofuata kwani ndio siku
ambayo mfungo unaanza.
“Mimi nauza mchele, bei ni Sh 2,000 hadi 2,200 ndio bei ambayo
imezoeleka hivyo huwezi kusema kwamba imepanda kwani sitegemei
kupandisha bei zaidi tunaweza kupunguza bei kwa kuwa ndio msimu wa
mavuno,” alisema Hassan.
Pia alisema kupanda kwa bei inategemea na msimu kwani kuna wakati
bidhaa zinakuwa zinapatikana kwa shida na mwezi wa Ramadhani unaanza
hivyo wanavyopandisha bei, watu wanasema wamepandisha sababu ya mfungo.
Mfanyabiashara wa viazi sokoni hapo, Zainabu Suleiman alisisitiza
kuwa bei hizo hazijapanda kwa kuwa bado wanauza fungu moja Sh 1,000 na
Sh 2,000. Alisema mazao mengi ya vyakula ndio msimu wake na kusisitiza
kuwa wakiongeza bei hizo watapata dhambi kwa kuwa watu wanaofunga
hawapaswi kuteseka na bei.
“Njoo Jumatano au Alhamisi labda bidhaa hizi zinaweza kupanda bei
lakini hadi leo bado hazijapanda. Mfano magimbi, hapa tunauza kwa fungu
Sh 1,000 hadi Sh 2,000 ni bei ya kawaida kwa kipindi chote hiki,”
alieleza Zainabu.
Aidha, katika soko la Buguruni, bei za bidhaa hizo hazijapanda huku
mazao mbalimbali ikiwemo muhogo kutoka mashambani ikishushwa kwa wingi
na bei yake ni Sh 1,000 hadi 2,000 kwa fungu. Wafanyabiashara wa masoko
hayo wamesema kuwa bidhaa hizo zitaendelea kufurika kwenye soko hilo
kuanzia leo.
Post your Comment



