MVUTANO kuhusu uendeshaji wa Bunge unaoendelea kati ya wabunge wa CCM
na wa vyama vya upinzani, umeibukia kwenye semina za mafunzo ya
wabunge, baada ya wabunge wawili kutoka vyama tofauti kuonesha tofauti
zao kisiasa.
Hali hiyo ilijitokeza kwenye semina kuhusu mbinu za wabunge
kufuatilia matumizi ya fedha za umma, ambayo miongoni mwa watoa mada
alikuwa Dk Colman Msoka, kutoka Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS) ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mvutano huo uliibuka kati ya Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini
(Chadema) na Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwako (CCM) wakati
wakichangia mada mbalimbali zilizotolewa kuhusu ufuatiliaji wa matumizi
ya Serikali. Akichangia, Selasini alisimama na kusema Bunge la sasa
limegeuka mhuri wa kupitisha kila kitu kutoka serikalini.
Akitumia uzoefu wake kuwa mbunge wa vipindi viwili, kwa maana ya
2010-2015 na sasa 2015-2020; Selasini aliwaambia wabunge hasa walio
wapya kuwa anaona tofauti kubwa ya Bunge lililopita na la sasa.
“Tukazanie kuimarishwa kwa demokrasia ya Bunge la sivyo tunakokwenda
Bunge litafutika…mimi ni mbunge wa vipindi viwili, naweza kufananisha
Bunge lililopita na hali ilivyo katika Bunge la sasa,…la sasa ni mhuri,”
alidai.
Alidai kuwa wakati kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali,
kinachoonekana kwa sasa wabunge wanaiogopa. Alisema kama hali hiyo
itaendelea, hakuna haja ya wao kuendelea kuwa wabunge. Kwa mujibu wa
Selasini, katika uandaaji wa bajeti, wataalamu hasa wa Hazina wamekuwa
wakijiona ndio wenye uwezo kuliko wabunge na kwamba ndio maana
hawachukui maoni yao.
Kauli hiyo ya Selasini ilimuinua Nsanzugwako, ambaye alimtaka mbunge
huyo wa Chadema aache kupotosha wabunge wapya akisema wabunge ni zao la
vyama vya siasa na vyama vya upinzani vina majukumu tofauti na chama
tawala. Nsanzugwako ambaye hii ni mara yake ya pili kuwa Mbunge, alisema
vyama vya upinzani vilishindwa katika uchaguzi mkuu, hivyo havina
ajenda lakini vina kazi ya kufanya ambayo ni kukosoa Serikali.
Alisisitiza umuhimu wa chama tawala kupewa nafasi ya kutekeleza
ajenda yake kwa kuwa ndio kilichoshinda Uchaguzi Mkuu. Alishauri
kuandaliwe pia mafunzo kuhusu kazi za chama chenye Serikali na chama cha
upinzani. Kuhusu kuimarisha kazi ya Bunge katika usimamizi wa Serikali,
Nsanzugwako aliwataka wabunge kujenga uhusiano bila kujali vyama
uwawezeshe kufanya kazi ya Bunge.
Alihadharisha kuwa bila uhusiano wa wabunge katika ufuatiliaji wa
bajeti, wataishia kutunishiana misuli bungeni kati ya chama tawala na
vyama vya upinzani. Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Mbunge wa Sumbawanga
Mjini na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Aeshi Hilaly (CCM), alisema kamati anayoiongoza na Bunge
kwa ujumla, haviwezi kushikiliwa na Serikali.
Alisema ili kuimarisha kamati ambazo zinategemewa kutoa taarifa kwa
Bunge, chombo hicho kiliona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo wabunge
waelewe umuhimu wao katika kufuatilia bajeti ya Serikali. Aeshi alisema
kama Kamati ya Bunge ikiwa dhaifu na Bunge litakuwa dhaifu kwa kuwa
itapeleka taarifa dhaifu na kufanya Bunge kushindwa kutekeleza wajibu
wake ipasavyo.
Alisema ndiyo maana mafunzo hayo yamehusisha wajumbe wa PAC, Kamati
ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) na Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Akizungumza katika mafunzo hayo, mmoja wa watoa mada, Dk Msoka,
kutoka Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS) ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, alisema utafiti umeonesha kuwa kamati za Bunge zinapokuwa
madhubuti, pia Bunge huwa madhubuti.
Wakati huo huo, Bunge linaendelea leo, ambapo baada ya maswali na
majibu wabunge wataendelea kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Serikali
na kutoa maoni kuhusu Mpango wa Serikali wa 2016/2017.
Post your Comment



