HATUA ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo)
kuanzisha mjadala wa bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha nje ya
Bunge, imekosolewa ukitajwa kwamba hauna tija zaidi ya kuwavuruga
wananchi.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa, waliohojiwa jana,
walisema kitendo hicho ni mkakati usio na tija huku wengine wakisema ni
maoni ya kujifurahisha. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk
Benson Bana alisema kitendo hicho cha Zitto ni ‘mkakati usio na tija’.
Naibu Katibu wa Bunge, John Joel alisema ‘ni maoni ya kujifurahisha’
wakati Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alisema atajitokeza
hadharani baadaye kutoa maoni ya kuliunganisha Taifa.
Baada ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge hivi karibuni
kutokana na kukiuka taratibu, Zitto amekuwa akitumia majukwaa kukosoa
bajeti na Serikali ya Rais John Magufuli, hatua ambayo imeelezwa pia
kuwa inashusha heshima ya Mbunge huyo. Warioba kufunguka Warioba ambaye
alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, alipotakiwa kutoa
maoni yake kwa hatua hiyo, alisema wakati utakapofika atajitokeza na
kueleza namna wanasiasa wanavyotumia vibaya nafasi zao za kisiasa.
“Kwa sasa tumekaa kimya, lakini wakati utafika ambapo tutajitokeza na
kutoa maoni yetu kwa maslahi mapana ya taifa pamoja na kwamba tunaona
namna wanasiasa wanavyotumia vibaya nafasi zao za kisiasa na kuligawanya
Taifa. Kazi yetu sisi ni kuliunganisha taifa kuwa moja,” alisema Jaji
Warioba.
Mhadhiri amshangaa Zitto Kwa upande wake, Dk Bana akizungumza na
gazeti hili jana alisema; “ Zitto alipaswa kukusanya maoni ya wananchi
ili kuyapeleka bungeni.” “Wakati serikali ilipokuwa inaandaa bajeti yake
ya mwaka huu na hata Mpango wa Taifa wa Maendeleo, Zitto alipata fursa
ya kushiriki maandalizi yake katika hatua mbalimbali akiwa Mbunge.
“Ni wakati huo ndipo Zitto alipaswa kukusanya maoni ya chama chake au
makundi mengine ya kijamii wakiwemo wananchi wake ili baadaye
ayawasilishe serikalini au bungeni ili kuwezesha kupatikana kwa bajeti
bora na si hatua hii anayoichukua sasa,” alisema Bana.
Alisema Mbunge huyo pamoja na kuzijua fika taratibu za Bunge, aliamua
kwa makusudi kuzikiuka na hivyo kupoteza dhamana aliyokabidhiwa na
wananchi ya kuwawakilisha ndani ya Bunge ili kujadili masuala yenye
maslahi mapana kwa taifa ikiwemo bajeti na sasa amebuni mkakati usio na
tija.
Alisema pamoja na kufahamu umahiri wa mbunge huyo katika medani ya
siasa hatua ambayo iliwezesha wananchi kuwa na imani kubwa na
mustakabali wake kisiasa, kwa bahati mbaya Mbunge huyo amepoteza
mwelekeo na kuanza kutoa kauli alizosema hazina manufaa kwa wananchi.
“Anachoendelea kukifanya Zitto ni mwendelezo wa kile alichokifanya
Mbagala alipotoa lugha ya kuudhi dhidi ya Rais (John Magufuli). Wote
tunajua mambo ya bungeni yanajadiliwa bungeni. “Haiwezekani leo
mwanasiasa anayejiita mahiri anaitisha mjadala kuhusu bajeti wakati
hotuba ya bajeti ikiwa mezani na wananchi wakifuatilia mjadala wake
bungeni, huku ni kuwavuruga wananchi na si jambo la msingi kwa taifa,”
alisema Profesa Banna.
Akizungumzia mwelekeo wa kisiasa kwa Mbunge huyo wa Kigoma Mjini,
Bana alisema pamoja na kuaminiwa kuwa na sauti yenye ushawishi na mvuto
wa kisiasa, lakini wasomi wamekuwa wakimchukulia Zitto kama mwanasiasa
anayeanzisha hoja na kuziacha hewani bila kuzimaliza.
“Ni tofauti na Kafulila (David- Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini).
Zitto anapenda kuanzisha hoja na kuziacha zikielea. Kila siku anakuja na
hoja mpya, mara bajeti, mara fedha zilizofichwa nje, mara Escrow, mara
rais hivi. Ni mtu ambaye hoja zake zinafichwa na ajenda binafsi nyuma
yake,” alisema Bana.
Ofisi ya Bunge yafafanua Kwa upande wake, akitoa maoni kuhusu msimamo
wa Bunge kwa hatua hiyo ya Mbunge Zitto kuhamishia mjadala wa bajeti
nje ya Bunge, Naibu Katibu wa Bunge , John Joel alisema pamoja na kuwa
kitendo hicho hakizuiliwi, lakini hakina tija kwa wananchi.“Zitto anaendesha mjadala ili apate maoni ya kumpelekea nani?”
Alihoji Joel na kusema kuwa Mbunge huyo angeweza kukubalika zaidi endapo
angetumia jukwaa la Bunge kujadili kile anachokiona katika bajeti ya
serikali kwa mwaka ujao wa fedha.
Naibu Katibu huyo wa Bunge alisema kinachoshangaza zaidi ni kuona
kuwa mkakati huo wa kujadili bajeti, hata pale unapoonekana kuvalishwa
joho la chama cha ACT – Wazalendo ambapo Zitto ni Kiongozi Mkuu, lakini
haufanywi kwa vikao vya ndani vya chama na badala yake unaelezwa kuwa ni
mjadala wa wazi, hatua inayochanganya wananchi.
Post your Comment



