UDHAIFU wa Kanuni za Bunge katika kufafanua mambo mbalimbali ya
uendeshaji wa Bunge, umeelezwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwa
unatakiwa kurekebishwa ili kutoa nafasi ya Kiti cha Spika kutoa uamuzi
dhidi ya vitendo visivyokubalika vinavyoendelea ndani ya Bunge.
Amesema hayo jana alipokuwa akitoa majibu wa muongozo alioombwa na
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge Nkasi
Kaskazini, Ally Keissy (CCM) kuhusu uhalali wa posho wanazolipwa wabunge
wa Kambi ya Upinzani, ambao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na
kwenda kupumzika.
Dk Tulia alisema tangu Mei 30, mwaka huu, wabunge hao wamekuwa
wakiingia bungeni kusaini posho na kuondoka kwenda kupumzika, jambo
lililosababisha Dk Mwakyembe kuomba muongozo kama malipo hayo ni haki
kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya Katiba ya 23.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 23, ibara ndogo
ya kwanza na ya pili; “Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote,
anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote
wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na
kiasi na sifa za kazi wanayoifanya.
Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.” Akitoa
muongozo wake kama malipo hayo ya posho ni halali kwa mujibu wa Katiba
au la, Naibu Spika alisema ametumia uamuzi wa Kiti cha Spika uliotolewa
Aprili 27, 2016 kuhusu muongozo kama huo.
Alisema Kiti cha Spika katika muongozo huo wa Bashe, kilinukuu Katiba
Ibara ya 73 inayosema, “Wabunge wote wa aina zote watashika madaraka
yao kwa mujibu wa Katiba hii, na watalipwa mshahara, posho na malipo
mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”
Mbali na malipo hayo kulindwa na Katiba, Dk Tulia alisema pia Sheria
ya Uendeshaji wa Bunge Sura ya 15 na 19 Kanuni za Bunge zinaelezea kuwa
mbunge anapohudhuria vikao vya Bunge, atalipwa posho.
Dk Tulia alisema vitendo vya kutohudhuria mjadala wa Bunge
havikubaliki kwa kuwa havikidhi matakwa ya Katiba Ibara ya 23, lakini
akasema pamoja na Kiti cha Spika kusisitiza kuwa kutohudhuria mjadala
hakukubaliki, lakini kuna haja ya kubadili sheria ili mbunge alipwe
baada ya kumaliza kazi.
Pia alisisitiza kuwa Kanuni za Bunge zinazotumika katika kuwalipa
posho, hazijaeleza kwa uwazi maana ya neno mahudhurio, hivyo nazo
zinahitaji marekebisho kudhibiti hali hiyo.
Baaada ya kutoa muongozo huo, Keissy alisimama na kuomba muongozo
mwingine na alipopewa nafasi, aliomba utaratibu wa kutumia mashine za
kielektroniki kusaini mahudhurio, ubadilishwe na badala yake urejeshwe
ule wa zamani wa mbunge kusaini katika karatasi.
Dk Tulia akijibu muongozo huo, alisema hata ukirejeshwa utaratibu
huo, mbunge anaweza kusaini katika karatasi saa tano na kuondoka kwenda
Dar es Salaam na kusisitiza kunahitajika marekebisho ya Kanuni za Bunge
ili neno mahudhurio, lipewe ufafanuzi wa wazi.
Hata hivyo, aliahidi kuwasiliana na Katibu wa Bunge ili kuona
utaratibu mzuri wa wabunge kusaini posho katika wakati wa sasa. Baada ya
muongozo huo wa Naibu Spika, Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi maarufu Sugu alidai wao wataendelea kususia vikao vyote vya
Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika kwa madai kuwa anatumia Kanuni za
Bunge, kuwakandamiza.
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa
Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni,
Mbilinyi alisema wabunge wa Kambi ya Upinzani wanaposusa hawarudi
nyumbani kupumzika, bali wa wanashinda katika maktaba ya Bunge kufanya
kazi.
Mbilinyi alisema ni heri wabunge wa Kambi ya Upinzani wanaoshinda
katika maktaba ya Bunge, kuliko wa CCM wanaohudhuria vikao hivyo. Gazeti
hili lilitembelea katika maktaba hiyo ya Bunge kuthibitisha kauli ya
Mbilinyi na kumkuta Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM) peke yake
akifanya kazi za kibunge na mtumishi mmoja wa Bunge.
Post your Comment



