Waziri mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba
Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa tatizo la uhaba wa sukari
nchini ambapo jumla ya tani 20,000 zilisambazwa jana katika maeneo
mbalimbali nchini.
Amesema shehena nyingine ya tani 35,000 inatarajiwa kusambazwa
hivi karibuni katika kanda zote nchini hivyo amewataka wafanyabiashara
watakapoipokea kuiuza kwa wananchi bila ya kuificha na bei isizidi
shilingi 2,200.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jana jioni ( Ijumaa, Juni 10,
2016) wakati akizungumza na Masheikh na Viongozi wa Kamati ya Amani ya
mkoa wa Dar es Salaam alipowaalika katika futari aliyoiandaa nyumbani
kwake.
Amesema tayari viwanda vimeanza kufunguliwa na tani 300 zilizotoka
katika kiwanda cha Sukari cha Kagera zitasambazwa katika wilaya za
Kakonko, Kibondo, Kasulu, Uvinza na Kigoma ili kutosheleza maeneo hayo.
Hata hivyo amewataka Maofisa Biashara katika Halmashauri zote
nchini kuendelea kufanya ufuatiliaji katika maduka ili kuhakikisha
bidhaa hiyo inapatikana na hakuna mfanyabiashara atakayeificha.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara kote
nchini kutopandisha bei za vyakula katika kipindi cha mfungo wa Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza kuhusu tabia za baadhi ya wafanyabiashara wanaopandisha
bei za bidhaa hasa vyakula katika kipindi hiki cha mfungo amewataka
kumuogopa Mwenyezi Mungu kwa sababu kitendo hicho kinawapa wafungaji
wakati mgumu.
“Kufunga Ramadhani si jambo la anasa, si matashi binafsi bali ni
jambo la kiimani hivyo tusipandishe bei ya bidhaa kwa lengo la
kuwaadhibu Waislam kwa sababu tu wamefunga.
“Katika Quran surat Baqarah aya ya 183 inasema kwamba enyi
mlioamin imefaradhishwa kwenu kufunga kama walivyoamrishwa kufunga kwa
waliopita kabla yenu ili muwe wachamungu, hivyo hatuna budi kufunga”
alisisitiza.
Alisema tabia hiyo si nzuri na imekuwa ikijitokeza mara kwa mara
unapofika wakati wa mfungo kwa wafanyabiashara kuamua kupandisha bei
hivyo aliwataka waiache kwani Serikali haitawavumilia na atakayethubutu
hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Post your Comment



