MAFANIKIO yaliyoonekana katika programu ya Kusoma, Kuandika na
Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa madarasa ya chini, yamewavutia wadau
mbalimbali wa elimu na kuahidi kutoa Sh bilioni 75 kwa ajili ya
kuimarisha stadi hizo.
Akizindua taarifa ya kupima uwezo wa watoto kupitia programu hiyo Dar
es Salaam jana, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa
Joyce Ndalichako alisema utafiti uliofanywa mwaka huu umeonesha kuwa,
uwezo wa watoto katika mambo hayo matatu unaonekana kukua katika viwango
tofauti kiasi cha kuridhisha.
Aliongeza kuwa, stadi hiyo ilifanyika katika shule 650 nchini na
kujumuisha watoto 7,000 ambapo baada ya uzinduzi huo, taarifa hiyo
itachambuliwa zaidi na wataalamu ili kuongeza mafanikio zaidi katika
mambo hayo.
Alisema wakati inaanza programu ya Matokeo Makubwa Sasa, ilionekana
suala la watoto kutojua kusoma, kuhesabu na kuandika ni tatizo kubwa,
hivyo ikawekwa mikakati ya kuongeza ufundishaji kuondokana na tatizo
hilo.
Mkakati wa Serikali ni kuinua ubora wa elimu ambapo itajenga misingi
mizuri zaidi na kwamba tayari wamechapisha vitabu vitakavyosambazwa nchi
nzima na pia itatoa mafunzo kwa wakaguzi wa elimu, walimu na waratibu
wa elimu.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na Shirika la Kimataifa la
Research Triangle International (RTI) wakishirikiana na Data Vision, kwa
msaada wa USAID watoto wa kike wameonekana kufanya vizuri zaidi ya
wenzao wa kiume.
Post your Comment



