WAKATI kesho Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikitarajiwa
kutimiza azma yake ya kuzima simu ‘feki’ za mkononi, upo mtikisiko na
kizaazaa miongoni mwa watumiaji wa vifaa hivyo vya mawasiliano, wakisaka
mbadala na wengine wakisubiri kuona kama ‘yatatimia’.
Ingawa uzimaji wa simu bandia na kuanza kutumika kwa teknolojia mpya
ya simu za mkononi kwa Mfumo wa Rajisi, unatarajiwa kuwa muarobaini wa
wizi kwa simu za mkononi na kiama kwa watukanaji, watumaji picha chafu,
baadhi ya wanajamii wanaipokea hatua hiyo kwa mtazamo hasi, wakiangalia
hasara watakayopata baada ya simu zao kufungiwa.
Kizaazaa kimekumba siyo tu watumiaji wa simu, hususan wale ambao
wameshabaini kuwa simu zao ni bandia, bali pia wenye maduka ya simu
ambao baadhi inadaiwa kusafirisha simu hizo kwenda kuziuza nchi jirani.
Wakati hayo yakijiri miongoni mwa watumiaji wa simu za mkononi, kwa
upande wao, kampuni za simu za mkononi zimetumia fursa hiyo kufanya
biashara ya simu za mkononi kwa bei nafuu, itakayowezesha wenye kipato
cha chini kumudu bei yake.
Baadhi ya wafanyabiashara wa simu jijini Dar es Salaam walieleza matamanio yao ya kuzimwa simu bandia ili
biashara yao iendelee, kwa kile walichosema imedorora tangu TCRA
ilipotangaza uamuzi wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema kumekuwa na hofu
miongoni mwa wateja ambao wengi wanachelea kununua simu kutokana na hofu
ya kuuziwa zilizo bandia.
“Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, biashara ya simu imeyumba kwa kiasi
kikubwa kutokana na tangazo la TCRA,” alisema Mohammed Bakari ambaye
hata hivyo alisema binafsi anauza simu halali, ambazo pia zimekosa soko
kama ilivyo kawaida kutokana na kuhofia za bandia.
Mfanyabiashara mwingine, Erick Ngamwe alisema, uamuzi wa serikali wa
kuzima simu hizo ni jambo zuri. Alishauri isitoe muda wa ziada ambao kwa
mujibu wake, utaendelea kuyumbisha biashara yao.
Hata hivyo, mfanyabiashara mwingine wa Kariakoo, Nassor Said alisema,
wapo baadhi yao ambao wataumia kwa kuwa walikuwa na mzigo mkubwa wa
bidhaa hiyo.
“Hili tunaliona jambo zuri lakini kuna watu wanaumia, watu walikopa
fedha kuagiza mzigo wa simu leo hii hajamaliza hata kerejesha pesa yote,
simu zinazimwa na anakuwa anapata hasara, kwahiyo si jambo la
kufurahia,” alisema Said.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliohojiwa juu ya hatua hiyo
inayotarajiwa kutekelezwa kesho, waliomba muda uongezwe huku walilaumu
kitendo cha mamlaka zinazohusika kufumbia macho uingizaji wa simu bandia
kuwa ni adhabu kwa watu wenye kipato cha chini.
Hata hivyo katika maeneo mbalimbali, mwandishi alishuhudia umakini
kwa wanaonunua simu ambao wengi walikuwa wakilazimika kutumia kanuni
iliyotolewa na TCRA, kubaini kama simu anayonunua ni bandia au halisi.
Wakiwa kwenye gulio la simu lililoandaliwa na kampuni za simu jijini
Dar es Salaam hivi karibuni, walionekana watu wengi waliokuwa wakinunua
simu za gharama nafuu huku wakihoji maswali kuhusu uhalali wake. Kampuni
zatoa ofa Kampuni zinazotoa huduma za simu zimesema zinaendelea
kusambaza simu za gharama nafuu nchini na kutoa ushauri kwa wateja .
Alipohojiwa juu ya athari watakazopata wateja wenye simu feki baada
ya simu zao kuzimwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa
Vodacom Tanzania, Rosallyn Mworia alisema laini za wateja
hazitaathirika, bali simu bandia wanazotumika ndizo hazitafanya kazi.
Wakati huo huo kampuni ya simu ya Airtel imetangaza ofa kwa watu
wanaohitaji simu halali, kuendana na matakwa ya serikali ya wananchi
wake kutumia simu zinazokubalika kiafya na zenye ufanisi mkubwa.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana, kampuni hiyo imesema Airtel
Tanzania imeanzisha ofa ya kununua kifurushi chenye thamani ya Sh 22,000
kupata simu ya bure.
Mkuu wa kitengo cha Intaneti, Gaurav Dhingra alisema: “Tunatambua
kwamba baadhi ya wateja wetu bado wanatumia simu ambazo hazina uhalisia,
hivyo wako katika hatari ya kuzimiwa simu zao hapo itakapofika siku ya
Alhamisi, Juni 16 (kesho).”Wizi wa simu basi
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari na wafanyabiashara
wa maduka ya simu mjini Kigoma jana, Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati wa
TCRA, Esuvatie Masinga alisema teknolojia hiyo itasaidia kudhibiti wizi
wa simu za mkononi nchini.
Alisema simu itakayoibwa na kutolewa taarifa, itafungwa na haitaweza
kutumika mahali popote duniani. Alisema teknolojia hiyo itadhibiti
matumizi mbalimbali yasiyofaa ya simu za mkononi, ikiwemo wanaotukana,
wanaotuma picha chafu na matumizi mengine yanayokatazwa.
Masinga alisema simu inapoibwa, utambulisho wa simu hiyo utaonekana
kwenye laini nyingine itakayowekwa iwapo simu hiyo itaendelea kutumika.
Mtu aliyekuwa na simu hiyo, atafuatiliwa na kukamatwa.
Sambamba na hilo, Meneja huyo alisema kuwa mfumo huo, unatoa faida
kwa wanunuzi wa simu, ambao watapaswa kupewa garantii ya mwaka mmoja ya
matumizi, jambo linalowalazimisha wafanyabiashara wanaouza simu kuuza
simu halisi na siyo bandia.
Meneja huyo wa TCRA alisema simu zote na vifaa vyote vya mawasiliano
ambavyo ni bandia, vitazimwa kama ambavyo imeshatangazwa awali na hakuna
muda wa nyongeza kwa simu bandia kuendelea kutumika.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emanuel Maganga
alisema udhibiti wa Mfumo wa Rajisi wa Simu za Mkononi, utasaidia
kudhibiti uuzwaji wa simu holela, ambao unachangia kuwafanya
wafanyabiashara kukwepa kukodi.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa alishauri bei za simu iwe ambayo wananchi
wote watamudu. Aliomba mamlaka isimamie hilo, kuhakikisha
linatekelezeka.
Post your Comment



