WABUNGE wa kambi ya upinzani waliosusa vikao vya Bunge,
vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Tulia Ackson, wameendelea kubanwa,
wakiambiwa kuendelea kufanya hivyo ni kutofahamu wajibu wao wa
uwakilishi kwa wananchi.
Watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wa vyama vya siasa
na baadhi ya wabunge wa CCM, wamewataka hao wenzao waliosusa, kutengua
msimamo wao, warudi bungeni kuleta afya katika mijadala.
Miongoni mwa waliozungumzia hilo ni Mbunge wa Mtera (CCM),
Livingostone Lusinde, aliyesema wapo baadhi ya wabunge wa upinzani,
wamemhakikishia kuwa wako tayari kuingia bungeni lakini wanashindwa
kufanya hivyo kwa kuzuiwa na Kiongozi wa kambi hiyo bungeni, ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe.
Askofu wa Kanisa la Methodist Tanzania Jimbo la Dodoma, Joseph
Bundala alisema kitendo wanachofanya wabunge hao wa upinzani ni kutojua
wajibu wao kama wawakilishi wa wananchi.
Akihubiri kwenye ibada ya Jumapili iliyopita katika kanisa hilo
ililopo Ipagala Manispaa ya Dodoma, askofu huyo alisema wanadhihirisha
kuwa wachanga kidemokrasia.
Askofu Bundala alisema, kususia vikao vya Bunge vinavyoongozwa na
Naibu Spika, Dk Tulia hakuna maana bali wanachotakiwa kufahamu ni
kwamba, wanapaswa kuchangia mijadala kwa ajili ya wananchi
waliowachagua.
“Kama kiongozi wa dini, nawasihi wabadilike haraka kutoka katika hali
ya uchanga na kufikiria utimilifu wa kidemokrasia,” alisema na
kusisitiza kuwa kufanya hivyo, watatenda haki kwa wananchi waliowatuma.
Wakati huo huo aliwataka kuacha kulisema vibaya Jeshi la Polisi, lenye
jukumu la kulinda amani na utulivu. Alisisitiza hakuna nchi isiyoongozwa
na sheria.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mtera, Livingostone Lusinde (CCM) alisema
wabunge wengi wa upinzani wamemhakikishia kuwa wako tayari kuingia
bungeni lakini wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu wanazuiwa na
kiongozi wa kambi hiyo ya upinzani, Mbowe.
“Wako hapo kwenye chai, wamenituma nije niwasemee kwamba wako tayari
kuingia bungeni lakini Mbowe anawapigia simu na kuwazuia wasiingie. Hata
hivi ninavyoongea watakuwa wananipigia makofi kwa kuwasemea,” alisema
Lusinde bungeni jana.
Akichangia Bejeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/15 na hali ya
uchumi kwa mwaka 2015, Lusinde alimshauri Mbowe kuacha udikteta ili
wabunge hao watoe mchango wao katika mjadala wa bajeti unaoendelea.
Hata hivyo, alisema kwa vile CCM ndicho chama mama, ni vyema wabunge
wa chama hicho wakajadili hata kero za majimbo yanayoongozwa na ya
wapinzani bila kubagua kwa faida ya Watanzania wanaoishi katika majimbo
hayo.
Aliitaka serikali isiruhusu wapinzani kuendeleza siasa hata baada ya
kampeni kumalizika kwa sababu wanasababisha vurugu katika kipindi
ambacho serikali ina mambo mengi ya kufanya kwa ajili ya kuwapatia
wananchi maendeleo.
“Kwa mfano, kama Mbowe analalamika kuhusu mambo yaliyotokea bungeni
kwa nini asiende kwenye jimbo lake la Hai na badala yake anataka kwenda
Kahama kwa Mheshimiwa Jumanne Kishimba. Hii ni fujo,” alisema na
kuvitaka vyombo vya dola visiruhusu watu wasiopenda utulivu kwa sababu
nchi haiwezi kuwa mwaka mzima inaendesha siasa za majukwaani.
Akigusia hoja hiyo wakati akijadili bajeti, Mbunge wa Kasulu mjini
(CCM), Daniel Nsanzugwanko alishauri uongozi wa Bunge na wabunge wa CCM,
watafute mwafaka kwa kuwasamehe wabunge wa upinzani ili warudi bungeni.
“Sisi (CCM) ni chama kikubwa na hatufaidiki na huu mgomo wa
wapinzani. Tuwasamehe, tuwahurumie ili kumaliza hii stalemate
(mgogoro),” alisema.
Hata hivyo, wakati akiahirisha shughuli za Bunge jana mchana, Naibu
Spika, Dk Tulia Ackson alimjibu Nsanzugwanko kwamba hakuna aliyewatoa
bungeni wapinzani na wala hawajakosa lolote kuhitaji kusamehewa,
isipokuwa wanatoka nje kwa utashi wao.
Alirudia kusema kwamba kanuni zimeweka utaratibu mzuri wa nini cha
kufanya, pale mbunge anapokuwa hakubaliani na uamuzi wa kiti kwa
kuandika barua inayopelekwa kwenye kamati ya uongozi, jambo ambalo
hawajafanya.
Mapema, wabunge wengi wa CCM waliochangia jana, walianza kwa kusifia
utendaji wa Dk Tulia na kumtia moyo kwamba anaendesha vikao kwa weledi
na hawajaona kosa alilofanya.
Wakati huo huo, akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taifa
wa TLP, Augustino Mrema ametaka wabunge wa vyama vya upinzani,
waliosusia vikao kurudi bungeni. Aliwataka warudi bungeni na kufuata
demokrasia, badala ya kuachia mijadala yenye maslahi ya taifa ikiendelea
kujadiliwa wenyewe wakiwa nje ya Bunge.
Alisema kitendo cha kumkataa Naibu Spika Dk Tulia na kutoka nje
wakati akiwepo, hakifai kwa kuwa wanashindwa kuwawakilisha wananchi wao
waliowatuma.
“Kama hawamtaki Dk Tulia wangetumia demokrasia, sasa watatoka nje
hadi lini? Mi nawasihi warudi bungeni wafuate sheria, kanuni na
taratibu,” alisema.
Kiongozi huyo wa TLP alisema yeye ni mpinzani, lakini ni msema kweli
ambaye ataendelea kuwasema wasiotenda na kufuata haki na ambao ni
mafisadi.
Alisema baadhi ya wapinzani, siyo wa kweli na wamekuwa wakilalamikia
demokrasia kuvunjwa huku akiwashutumu kuwa wao wamekubuhu katika kuvunja
haki za binadamu, sheria, katiba na demokrasia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mrema alisema hali hiyo
ndiyo ilifanya upinzani kushindwa katika majimbo mengi, waliyokuwa
wakiyaongoza katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.
“Baadhi ya wapinzani siyo wakweli kabisa kama wanavyosema na wananchi
wanapaswa wawaelewe na wawe macho na kuwa makini na wanayowaambia. Kwa
sababu wamekuwa wakidai haki lakini siyo wanayowafanyia wengine,”
alisema.
Aidha Mrema aliwashutumu wapinzani kudai kwamba Rais Magufuli
anaendesha serikali bila kuzingatia haki za binadamu, hawatendei haki,
anavunja sheria na katiba, anawaonea na anaua demokrasia nchini.
“Wenyewe ndiyo vinara waliokubuhu kwenye vitendo hivyo kufanya hayo.
Huu ni unafiki mkubwa na wananchi wawe makini na wapinzani wa namna
hiyo,” alisema kiongozi huyo wa chama cha upinzani.
Post your Comment



