SERIKALI itawarudisha nchini Watanzania 500, waliokwama India baada
ya kampuni zilizowachukua kwenda kuwatafutia kazi, kukiuka mikataba yao
na kuwalazimisha kufanya kazi tofauti ikiwemo ukahaba.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mindi Kasiga aliyasema hayo jana Dar es Saalam wakati akizungumzia
matatizo wanayoyapata Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.
“Kati ya Machi hadi Mei 2016, balozi zetu nchini India na Malaysia
zimepokea maombi ya kusaidia kuwarejesha nyumbani Watanzania ambao
walipelekwa nchini India na Thailand kwa ahadi za kupatiwa ajira ambazo
hutolewa na watu wasio waaminifu ambao wanashukiwa kujihusisha na
mtandao wa biashara ya kusafirisha binadamu,” alisema Kasiga.
Alisema mtandao huo unawatafuta wasichana wenye umri kati ya miaka 18
hadi 24 na hata chini ya umri huo na kuwalaghai kuwa kuna fursa za
ajira katika hoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani nchi
za nje na kuwawezesha kupata hati za kusafiria na tiketi ya ndege kwa
ajili ya kusafiri kwenda kwenye nchi husika.
“Wengi huvutika kirahisi kwa kuona hiyo ni fursa ya kujipatia kipato
ila kwa taarifa tulizopata ni kwamba wengi hujua mapema kuhusu kazi
wanayoenda kuifanya huko ila ugumu wa maisha unapelekea kurubuniwa na
kuingia kwenye matatizo makubwa,” alifafanua msemaji huyo.
Alisema nchini India peke yake, kuna Watanzania takribani 500 wengi
wao wakiwa New Delhi (350), Bangalore (45), Mumbai (20) na wengine
wanaelekea Goa. Alisema kwa upande wa Mashariki ya Kati, kumekuwa na
wimbi kubwa la wasichana kurubuniwa kwa kutafutiwa fursa za kwenda
katika nchi za Oman, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu hasa Dubai kufanya
kazi za ndani.
“Baadhi ya wahanga wamekuwa wakikimbilia kwenye ofisi zetu za ubalozi
kuomba msaada na balozi zimekuwa zikiwahifadhi ubalozini na kisha
kuwasiliana na jamaa zao ili wawatumie nauli na kurejea nyumbani,”
alisema.
Alisema wizara imekuwa ikipokea maombi kutoka ofisi za ubalozi nchi
za Asia na Mashariki ya Kati ili kuwasaidia wasichana hao kurejea
nchini, na hivi karibuni kutoka Ubalozi wa Oman kulikuwa na wasichana 18
kati yao 10 wamesaidiwa kurudi na kuunganishwa na familia zao na
Ubalozi wa India wasichana 15 wamepeleka maombi yao.
Aliyataja matatizo yanayowakabili Watanzania nchi za Mashariki ya
Kati na Asia kuwa ni pamoja na kulazimishwa ukahaba na kunyang’anywa
hati za kusafiria ili kuwadhibiti wasitoroke na wengine kujikuta
kukubali kufanya ukahaba ili kurejesha gharama za kuwasafirisha pamoja
na kupata nauli.
Matatizo mengine ni kufanya kazi bila mikataba, kufanya kazi nyingi
ambazo zingetakia kufanywa na zaidi ya watu wawili au watatu, kufanya
kazi kwenye familia zaidi ya moja tofauti na makubaliano, kufanya kazi
bila muda maalumu wa kupumzika, kunyanyaswa na kubaguliwa na kufanyiwa
vitendo vya ukatili ikiwemo kupigwa, kutopewa fursa ya kuwasiliana na
mtu yeyote pamoja na kunyanyaswa kijinsia.
Alisema serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kutafuta majina
ya wahusika wote wa mtandao huo na kufanya mawasiliano na serikali za
nchi hizo ili kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika mkono wa sheria.
Post your Comment



