WASOMI nchini na wadau mbalimbali wameunga mkono Bajeti ya Serikali
ya mwaka 2016/17. Pia, wameunga mkono hatua ya serikali ya kuanzisha
mfumo wa kuwakata kodi wabunge katika malipo yao ya kiinua mgongo baada
ya kutumikia ubunge kwa miaka mitano.
Wamesema kama wabunge wataonekana wakati wa kuijadili bajeti hiyo,
wakipinga suala la kulipa kodi katika kiinua mgongo chao wanacholipwa
baada ya miaka mitano, watakuwa wabinafsi na siyo raia wema.
Walisema hayo walipokuwa wakitoa maoni yao kuhusu Hotuba ya Bajeti ya
Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, iliyowasilishwa bungeni mjini
Dodoma juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (pichani).
Walieleza kuwa maamuzi ya kuwataka wabunge kulipa kodi hiyo
yamechelewa, kwani kwa miaka kadhaa wamekuwa hawalipi kimakosa, kwani
wanalipwa fedha nyingi huku wananchi wanaopata mishahara midogo wakilipa
kodi.
Walieleza bayana kuwa ulipaji kodi unawahusu watu wote kuanzia rais
hadi mkulima hivyo wabunge walikuwa wakikosesha mapato halali ya
serikali. Ngowi, Bashiru, Bana walonga Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Mzumbe, Profesa Honest Ngowi alisema suala la wabunge kulipa kodi
limechelewa, kwani wengine wote wanalipa kodi na wao hawawezi kuwa juu
ya wengine.
Alisema kwa kuwa ni pendekezo la serikali na wabunge ambao ndiyo
wanatakiwa kupitisha, watajadili kutokana na kuwahusu kutakuwa na
mgongano wa kimaslahi, lakini iwapo watakataa watakuwa wabinafsi sana.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bashiru Ally
alisema kodi inakusanywa kwa lengo la kunufaisha watu wote kuanzia
ngazi ya rais hadi mkulima kulingana na vipato vyao, hivyo hakuna
mgogoro kwa wabunge nao kulipa kodi kwa mapato yao.
Dk Ally alisema anatarajia wabunge wataelewa na kuona ni haki yao
kulipana, ikiwa watajadiliana na kujenga hoja kwa lengo la kupata
msamaha wa kodi kama ilivyokuwa awali itaangaliwa hoja husika.
“Nasema ni msamaha kwani siyo haki yao kutolipa kodi ni lazima
kulikuwa na sababu na kama kuna mantiki kodi itaondolewa lakini kwa hoja
yenye mantiki vinginevyo hawana sababu ya kutokulipa kodi,” alieleza Dk
Ally.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Benson Bana akieleza kuwa suala la
wabunge kulipa kodi, licha ya kuwa limechelewa kutekelezwa, lakini kwa
mwaka 2020 wamewapa taarifa mapema.
Dk Bana alisema wabunge wamekuwa wakilipwa fedha nyingi, lakini
hawalipi kodi jambo ambalo walikuwa si raia wema kwani raia mwema
anatakiwa kulipa kodi kwa kile anachopokea.
“Ikiwa katika kujadili hotuba watatokea wa kupinga wataaibika kwani
hawatakuwa na sifa ya raia mwema ya kuunga mkono jitihada za serikali
kulipa kodi na watashangaza kwa kukwepa wajibu wao kwa kutotenda haki,”
alifafanua Dk Bana.
Waziri Mkuu IMTU aunga mkono Naye Waziri Mkuu wa Serikali ya
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya cha IMTU cha jijini Dar es
Salaam, Adili Msika alisema jana kuwa moja ya maeneo yaliyopongezwa na
wananchi wengi hususani wanafunzi ni hatua ya kuanza kukatwa kodi kwa
kiinua mgongo cha wabunge.
Msika alisema inashangaza kuona kuwa wakati wabunge wamekuwa
wakionesha kukerwa na wingi wa misamaha ya kodi na mianya ya kukwepa
mapato na kupunguza mapato ya serikali, lakini nao wamekuwa katika kundi
la watu wanaoshindwa kutimiza wajibu wa kulipa kodi halali za serikali.
“Wabunge kama wawakilishi wa wananchi na watunga sheria wanapaswa
kuwa mfano. Haiingia akilini kuona wabunge wanashiriki kutunga sheria za
kuwatoza kodi wananchi masikini wanaofanya kazi serikalini au
wanaofanya biashara ndogo ndogo huku wenyewe wakipewa kiinua mgongo bila
kukatwa kodi,” alisema Msika.
Alisema kutokana na ukubwa wa fedha za kiinua mgongo, ambazo wabunge
wamekuwa wakilipwa baada ya kukoma kwa kipindi chao cha ubunge cha miaka
mitano, serikali imekuwa inapoteza kiasi kikubwa cha mapato na kusema
wakati umefika kwa serikali kuanza kukusanya fedha hizo.
Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya
(TUGHE), Ally Kiwenge, akizungumzia hatua hiyo ya kuanza kukatwa kodi
kwa fedha za kiinua mgongo cha wabunge, alisema mpango huo lazima uungwe
mkono kwa sababu unatengeneza usawa.
“Hii ni hatua ya kuungwa mkono na kila Mtanzania. Nafahamu wabunge
watacharuka na kushinikiza mpango huo ufutwe, lakini wananchi na
wanaharakati ni lazima wasimame imara kuhakikisha kuwa hilo
linatekelezeka ili kuleta usawa,” alisema Kiwenge.
Kodi ya Majengo, Mahakama ya Mafisadi Aidha, Profesa Ngowi
alizungumzia ukusanyaji wa kodi ya majengo kufanywa na Mamlaka ya Mapato
(TRA) kuwa kama wameboresha mapungufu ya zamani, yaliyofanya kodi
kupelekwa katika halmashuri na kuwepo na utaalamu wa makadirio, basi
suala hilo litakuwa sahihi, lakini kama hakuna maboresho hakutakuwa na
jipya.
Aliitaka serikali na wabunge katika majadiliano, kuangalia suala la
utozaji kodi kwa sekta ya utalii ya asilimia 18, kwani Kenya ambayo ni
mshindani mkubwa wa sekta ya utalii inatoza asilimia 16 hivyo isije
kuathiri mapato.
Akizungumzia kutengwa fedha kwa ajili ya Mahakama ya Mafisadi, Dk
Ally alitaka iwe kwa muda na dharura kwa kuwa hali ya sasa ni mbaya,
lakini isiwepo mahakama kama ni kosa la kudumu, bali nchi iwekeze katika
mifumo imara ya uwajibikaji ili mafisadi wasipatikane.
Alisema kwa mifumo hiyo, itafanya nchi kuwa kama enzi za Mwalimu
Julius Nyerere ambako hakukuwa na watu wa kujilimbikizia mali, kwani
mafisadi ni watu wenye madaraka makubwa siyo watendaji wa kata ambao
wanaathiri maendeleo ya nchi.
Naye Dk Bana aliongeza kuwa licha ya kuwa bajeti ni nzuri, lakini
serikali ilitakiwa kuangalia vyanzo vipya vya mapato bila kutengeneza
bajeti yenye kumfikiria zaidi mwananchi wa mjini badala ya yule wa
vijijini na maeneo ya pembezoni.
Alisema ulipaji kodi ya majengo ni ya kikoloni ingeondolewa bila
kuathiri mapato kwa kutoza ya biashara pekee na siyo makazi kwani kuna
wastaafu wamejenga nyumba zao lakini wanakabiliwa na ulipaji kodi ambayo
hawana.
“Wakati serikali inahamasisha kuwa na nyumba bora lakini bado
wanatoza faini hivyo kurudisha nyuma jitihada za serikali ni vyema hili
la nyumba za kuishi kuangaliwa kwani ni usumbufu sana,” alieleza.
VAT za benki, simu yatia doa Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Fedha ya Dhow, Profesa Mohamed Warsame alisema pamoja na nia
njema ya serikali ya kuboresha maisha ya wananchi masikini, lakini hatua
ya kuanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye huduma za kibenki
na tozo kwenye huduma ya kutuma fedha kupitia simu za mkononi, kunaweza
kukuza gharama kwa wananchi.
Alisema katika kipindi hiki ambacho wananchi wanapaswa kupata huduma
za kibenki ikiwemo mikopo kwa urahisi na bila masharti magumu, hatua ya
serikali ya kuanzisha VAT kwenye mambo hayo mawili kunaweza kufanya
wamiliki wa benki kutumia nafasi hiyo kuwaumiza wananchi.
“Ni lazima serikali iliangalie hili suala kwa mapana yake. Ni vyema
mpango huu ukaenda sambamba na kuanzishwa kwa sera za udhibiti kwa benki
kutumia kisingizio hicho kupaisha gharama za benki na pia kampuni za
simu kutumia mwanya huo kuwaibia wananchi na kujinufaisha,” alisema
Profesa Warsame.
Aidha, alisema ni lazima pia serikali iwe makini na hatua ya kuanza
kutoza kodi ya asilimia 10 katika bidhaa za karatasi kwa vile hatua hiyo
inaweza kutia doa nia njema ya serikali ya kukuza kiwango cha elimu
nchini pamoja na sera yake nzuri ya kutoa elimu bure kuanzia darasa la
saba hadi kidato cha nne.
“Nasema hivi kwa vile wafanyabiashara hasa wale wanaochapisha vitabu
vya elimu au vijarida mbalimbali na hata wachapishaji wa magazeti
wanaweza kutumia mwanya huo kupandisha bei za uchapaji na kuongeza mzigo
kwa wananchi katika kupata vitabu na vijarida vya kielimu,” alisema.
CCM yataka vitendo Naye Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Christopher ole Sendeka amesema Watanzania watayafikia maendeleo
yanayokusudiwa katika mwaka mpya wa fedha, ikiwa watashiriki kuitekeleza
bajeti mpya kwa vitendo.
Kwa mujibu wa Ole Sendeka, bajeti hiyo imekuja na majibu ya kero
karibu zote za Watanzania hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha
inafanikiwa kwa kutoa ushirikiano unaostahili kupitia uwajibikaji katika
maeneo ya kazi, iwe kwenye sekta binafsi au serikalini.
“Bajeti ni nzuri na Watanzania hawana budi kukubali na kuelewa kuwa
wakati wote nchi inapoamua kuingia katika mabadiliko chanya ya kiuchumi,
haiwezi kufanya hivyo na kufanikiwa kwa mara moja, bali kwa hatua
inayohitaji ushiriki wa kila mmoja hasa katika uzalishaji.
“…Kwa maana hiyo, tunapaswa kuipa nafasi serikali huku tukiisaidia
kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha za umma, pamoja na uwajibikaji
katika uzalishaji na kulipa kodi zote zinazostahili kulipwa,” alisema.
“Hatua ya kufikia kuona kuwa taasisi za dini zinapaswa kulipa kodi
kwa bidhaa zinazoziingiza nchini italeta usawa miongoni mwa walipa kodi
kwa sababu wengi walikuwa wakizitumia kuingiza bidhaa zao kwa kupitia
msamaha wa kodi uliokuwepo, zipo taasisi za dini zinazojiendesha
kibiashara kupitia huduma za vyuo vikuu na nyinginezo, hizi zinastahili
kulipa kodi,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha DP, Abdul Mluye
alisema ushiriki wa wananchi kuitekeleza kwa vitendo ndio utakaowezesha
kuifanikisha. Mjadala kuhusu bajeti hiyo utafanyika kwa siku saba
kuanzia leo bungeni baada ya wabunge kutumia siku ya jana kusoma na
kutafakari hotuba ya Dk Mpango yenye thamani ya Sh trilioni 29.5.
Post your Comment



