WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali wa kufuta tozo tano
kati ya tisa alizokuwa anakatwa mkulima wa zao la korosho uko pale pale
na unatarajiwa kuanza kutumika katika msimu mwaka huu hivyo ameitaka
Bodi ya Korosho kusimamia uamuzi huo.
“Watendaji
wa Serikali katika ngazi mbalimbali mnatakiwa kuhakikisha kwamba
maelekezo haya yanafuatwa. Malengo yetu ni kumpunguzia mkulima mzigo wa
tozo nyingi alizokuwa anakatwa,” alisema.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Julai 16, 2016) wakati
akipokea taarifa ya maendeleo ya mkoa Mtwara pamoja na taarifa ya
kuondolewa kwa baadhi ya tozo katika zao la korosho zilizowasilishwa na
Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego.
Alisema
Serikali iliamua kuzifuta tozo hizo baada ya kubainika kuwa zilikuwa
zikiwanyonya wakulima hali iliyosababisha wauchukie mfumo wa stakabadhi
ghalani.
“Kuanzia
mwaka huu Serikali imeamua mfanyabiashara yeyote wa korosho hana budi
kuanza kulipa malipo ya awali kabla ya kuingia kwenye mnada ili tuwe na
uhakika wa kununua korosho hizo na kuwalipa wakulima kwa wakati,” alisema.
Akizungumzia
kuhusu changamoto ya kushuka kwa uzalishaji wa korosho Waziri Mkuu
aliutaka mfuko wa wakfu wa kuendeleza zao hilo ufanye utafiti wa kubaini
sababu ili waweze kutafuta namna ya kuipatia ufumbuzi.
“Nitakuja
kukutana na viongozi wa mfuko waniambie wanafanya nini na wamefanya
nini miaka mitatu iliyopita na wana mpango gani huko mbele tunakokwenda
kama hakuna mpango tutauangalia mara mbili mbili kwani wana fedha nyingi
lakini hata mbegu hawapeleki kwa wakulima,” alisema.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu aliitaka Bodi ya Korosho kuhakikisha kila
msimu wakulima wanapata pembejeo bora na zinawafikia kwa wakati ili
waweze kupata mazao ya kutosha.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 17, 2016
Post your Comment