TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania inahitaji wawekezaji kwenye
mashamba makubwa ya kibiashara pamoja na viwanda vya usindikaji mazao
ili iweze kuboresha uzalishaji nchini.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumapili, Julai 10, 2016) wakati akifungua
kongamano la siku moja la wafanyabiashara baina ya Tanzania na India
lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kufungua kongamano hilo
lililojumuisha wafanyabiashara 50 kutoka India ambao wameambatana na
Waziri Mkuu wa India, Bw. Narendra Modi, Waziri Mkuu Majaliwa alisema
Tanzania inayo fursa za uwekezaji kwenye sekta nyingi zikiwemo
miundombinu, kilimo, utalii, viwanda na madini.
“Serikali
ya awamu ya tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda lakini pia
imelenga kuzalisha malighafi za viwanda ambavyo tunahimiza vijengwe.
Lakini pia tumewaita waje kuwekeza kwenye sekta za uvuvi na utalii kwani
nazo bado hazijaendelezwa vya kutosha,” alisema.
“Tanzania
inazo kilometa 1,424 za fukwe za bahari, pia ina kilometa za mraba
223,000 za eneo la kiuchumi la bahari kuu (EEZ) na kilometa za mraba
54,337 za mito, mabwawa na maziwa ambayo ni sawa na asilimia 6.1 ya eneo
la nchi nzima. Kuna fursa nyingi kwenye uvuvi, usindikaji wa samaki na
ufugaji wa samaki kwenye mabwawa,” amesema.
Amesema
washiriki pia wamepata nafasi ya kusikia fursa za uwekezaji zilizoko
upande wa Zanzibar na kwamba kupitia vituo vya uwekezaji TIC na ZIPA
wanaweza kupata huduma zote palepale bila kuhangaika kwenye ofisi
mbalimbali.
Mapema,
akihutubia washiriki wa mkutano huo, Waziri Mkuu amesema kuna fursa
nyingine nyingi za kuwekeza kwenye sekta ya mifugo hasa katika
uanzishaji wa ranchi za mifugo, usindikaji wa maziwa na nyama,
usindikaji wa ngozi na utengenezaji wa bidhaa za ngozi.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu alisema urari wa kibiashara baina ya Tanzania na
India umeegemea upande mmoja ambapo India inauza zaidi bidhaa zake hapa
nchini Tanzania inavyouza bidhaa zake India. “Ninaamini njia mojawapo ya
kurekebisha hali hii ni kwa wafanyabiashara kutoka India kuamua
kuwekeza kwa kiwango kikubwa hapa nchini,” aliongeza.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mkutano huo, Waziri wa Viwanda na
Biashara, Bw. Charles Mwijage alisema Tanzania inahitaji India kama
ambavyo India inahitaji Tanzania katika kufanya biashara zake. “India
inaongoza kwa kuuza bidhaa zake hapa nchini lakini pia ni miongoni mwa
nchi 10 ambazo zinanunua kwa wingi bidhaa zake kutoka Tanzania,”
alisema.
Naye,
Rais wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda wa India (Federation
of Indian Chambers of Commerce and Industries - FICCI), Bw.
Harshavardhan Neotia alisema biashara kati ya Tanzania na India
inaendelea kukua na kwamba fursa zilizopo ni lazima zichangamkiwe
mapema. “Fursa za kibiashara ni kama mawio ya jua, ukiendelea kusubiri
sana unaweza usiyaone,” alisema.
Mkutano
umejadili mada mbalimbali zikiwemo fursa za uwekezaji Tanzania bara na
Zanzibar, fursa za uwekezaji kwenye maeneo ya kiuchumi, na uzoefu wa
baadhi ya wafanyabiashara kutoka India walioko nchini.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMAPILI, JULAI 10, 2016.
Post your Comment


