Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kuondoa ucheleweshwaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya
juu ili kuondoa migogoro kati ya wanafunzi na serikali yao.
Ameyasema hayo Jumanne hii jijini Dar es Salaam wakati akifunga
kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya chuo kikuu cha Dar es Salaam
ambapo alisema serikali inasimamia utendaji wa umakini na haitavumilia
tena ucheleweshwaji wa makusudi wa malipo ya fedha za mikopo ya elimu ya
juu.
“Sherehe kama hizi hutoa fursa kwa wahusika kutathmini kwa makini
mafanikio waliyoyapata na changamoto wanazopambana nazo katika kipindi
kilichopita ni fursa pia kufikiria maendeleo ya taasisi husika kwa siku
zinazofuata,”alisema Majaliwa.
“Serikali haitavumilia tena ucheleweshwaji wa makusudi wa malipo ya
fedha za mikopo ya chuo. Kama kuna tatizo, taarifa zitolewe haraka ili
kuzuia migogoro kati ya wanafunzi na serikali yao,”aliongeza.
Aidha Majaliwa amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuondoa
malimbikizo ya madai kwa watumishi wa umma na kwa sasa inakamilisha
uhakiki wa taarifa za watumishi ili kubaini watumishi hewa ambao hadi
sasa wamepatikana elfu 16,500.
Post your Comment