MAOFISA watano wa polisi wa Kenya wameuawa mapema jana mjini Mandera
katika shambulizi lililofanywa na wanamgambo wa Al-Shabaab kutoka
Somalia.
Kamishna wa jimbo hilo la kaskazini mashariki mwa Kenya, Job Borongo,
amethibitisha wapiganaji hao walifanya shambulizi la kuvizia dhidi ya
msafara wa magari ya polisi uliokuwa ukielekea El Wak wakitumia
guruneti.
Wakati maofisa wanne wakijeruhiwa vibaya, watano waliuawa papo hapo huku gari walilokuwa wakisafiria likiharibiwa.
Msafara huo wa polisi ulikuwa ukitoa ulinzi kwa msafara wa mabasi ya
abiria, utaratibu ulioanzishwa baada ya wapiganaji hao kuteka basi moja
na kuua abiria Wakristo 28.
Hata hivyo, Gavana wa Mandera, Ali Roba, aliwalaumu maofisa wa polisi
eneo hilo kwa kupuuza tahadhari iliyotolewa na wenyeji kuhusu
mashambulio ya kigaidi.
Roba alisema walipuuza vyanzo vya kiintelijensia kuhusu kuonekana kwa wapiganaji hao waliojihami kwa silaha.Hii si mara ya kwanza Mandera kushuhudia mashambulizi kutoka kwa Al-Shabaab.
Shambulizi lake la Novemba 2014 liliwaacha wasafiri wengi wasiokuwa
Waislamu na hofu ya kusafiri, na hivyo kuilazimu Serikali kutoa ulinzi
kwa mabasi ya uchukuzi wa umma.
Mwezi mmoja baadaye wapiganaji hao waliwaua wachimba madini 36 katika eneo hilo hilo.Kundi hilo limekuwa likitekeleza mashambulizi katika maeneo ya
kaskazini mwa Kenya likitaka kushinikiza taifa hili jirani kuondoa
majeshi yake Somalia.
Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi Somalia mwaka 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara nchini hapa.
Post your Comment



