BUNGE la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) limepitisha bajeti yake
ya mwaka 2016/17 ya Dola za Marekani milioni 100.1 (Sh bilioni 210)
ikiwa ni pungufu ya asilimia 10 ya bajeti ya mwaka jana wa 2015/16
ambayo ilikuwa ni Dola za Marekani milioni 111 (Sh bilioni 233).
Aidha, kupungua kwa bajeti hiyo kumetokana na baadhi ya wahisani
kupunguza misaada yao kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (ECA) huku
nchi wanachama zikishindwa kuchangia kikamilifu na ni nchi moja tu ya
Kenya ndiyo mpaka sasa imeweza kuchangia kwa asilimia 100.
Akizungumza jana baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Mwenyekiti wa
EALA, Abdullah Mwinyi wa Tanzania alisema kupungukiwa kwa asilimia kumi
ya bajeti ni pigo kubwa, hivyo wamejipanga vizuri kujitegemea katika
bajeti hiyo kulingana na kiasi walichonacho kwa kubuni njia bora za
mapato.
Hata hivyo, alisema licha ya changamoto hizo nchi wanachama zimekuwa
tatizo kubwa kwa kutotimiza ahadi zao kikamilifu za kutoa fedha kwa
wakati na pia kuwepo kwa nchi ya Sudan Kusini ambayo imejiunga katika
Jumuiya na nchi ya Burundi ambayo imekuwa na migogoro ya kisiasa suala
ambalo linaongeza changamoto katika Jumuiya hiyo.
Naye Spika wa Bunge hilo, Daniel Kidega wa Uganda, alisema Bunge
limepunguza bajeti kutokana na nchi wanachama kushindwa kuchangia kwa
wakati na wafadhili kupunguza bajeti yao ya utoaji misaada yao.
Post your Comment



