WAKATI
deni la Taifa likifikia zaidi ya Sh trilioni 35, Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk Phillip Mpango amesema Tanzania ina mahitaji makubwa ya
maendeleo yanayoilazimu kuendelea kukopa, kwa kuzingatia vigezo vya
kimataifa vya uhimilivu wa deni.
Akizungumza
mwishoni mwa wiki wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara hiyo
ya Sh trilioni 9.5, Dk Mpango alisema kwa kuwa lazima taifa likope ili
kuleta maendeleo, ni lazima taifa liwe na madeni.
“Nchi yetu ina mahitaji makubwa ya maendeleo hivyo lazima tukope na ukikopa, unaingia katika madeni,” alisema na kufafanua mambo ya msingi yanayozingatiwa na Serikali wakati wa kukopa.
Jambo
la kwanza wanalozingatia kwa mujibu wa Dk Mpango ni masharti ya mkopo,
yanayojumuisha riba ambapo wanaangalia riba hiyo ni kiasi gani; muda wa
kuanza kulipa baada ya kuchukua mkopo (grace period) na utaratibu wa
malipo.
Suala
la pili la msingi kwa mujibu wa Dk Mpango, ni mahali fedha hizo za
mkopo zinakopelekwa ambapo alifafanua kuwa ukopaji wa Serikali hauna
tofauti na ukopaji wa mtu binafsi, ambaye akielemewa anakaribisha
matatizo.
Dk
Mpango alisema Tanzania inakopa kwa ajili ya kutengeneza miundombinu,
akatoa mfano wa ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi na ujenzi
wa barabara nchi nzima, ambao mafanikio yake yasingefikiwa bila mikopo.
Pamoja
na kuendelea kukopa na deni kuwa kubwa, Dk Mpango alisema Serikali
hufanya tathimini ya kimataifa kuhusu uhimilivu wa deni kila mwaka ili
kujiridhisha na mpaka sasa pamoja na deni hilo kuonekana kubwa
kimataifa, Tanzania ina fursa ya kuendelea kukopa zaidi.
Tofauti
na inavyoelezwa kila mara na wanasiasa ambao wamekuwa wakichukua deni
la taifa na kugawanya kwa idadi ya watu, ili kupata fedha zinazodaiwa
kwa kila Mtanzania ikiwemo mtoto aliyezaliwa leo, Dk Mpango alitoa
vigezo ambavyo ni vya kimataifa kupima uhimilivu wa deni.
Vigezo
hivyo vinavyotumiwa kimataifa kupima uhimilivu wa deni, ni tofauti na
kigezo cha kugawanya deni kwa idadi ya watu ambacho ni cha kisiasa na
hakitumiki popote duniani isipokuwa kwa wanasiasa wa Tanzania.
Kigezo
cha kwanza cha kimataifa cha upimaji wa uhimilivu wa deni kwa mujibu wa
Dk Mpango, ni uwiano kati ya deni la taifa na pato la taifa, ambapo
kimataifa deni halipaswi kuzidi asilimia 50 ya pato la taifa na kwa
Tanzania, deni lipo asilimia 19 tu ya pato hilo.
Kigezo
cha pili kinachotumika kupima uhimilivu wa deni la taifa ni deni la
taifa kwa uwiano wa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi. Kimataifa,
deni la taifa halitakiwi kuzidi asilimia 200 ya mauzo ya nje na kwa
Tanzania, deni la taifa ni sawa na asilimia 97 tu ya mauzo ya huduma na
bidhaa nje ya nchi.
Kigezo
cha tatu kinachotumiwa kimataifa kupima uhimilivu wa deni la taifa kwa
mujibu wa Dk Mpango, ni uwiano wa deni la taifa na mapato ya ndani. Kwa
sasa kimataifa deni la taifa linatakiwa lisizidi asilimia 300 ya mapato
ya ndani na kwa Tanzania, deni hilo la taifa ni asilimia 145.3 tu ya
mapato ya ndani.
Post your Comment



