Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka
jeshi la Polisi kutumia mbinu za medani linapokabiliana na matukio ya
uvunjifu wa amani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanawanyanganya
majambazi silaha kabla ya kutekeleza uhalifu wowote.
Rais Magufuli amesema hayo wakati wa uzinduzi wa kituo cha
mawasiliano cha Jeshi la Polisi ambacho kitarahisisha utoaji wa taarifa
za uhalifu na kuharakisha askari polisi kufika katika eneo la tukio.
Kituo hicho cha kwanza kuanzishwa na Jeshi la Polisi hapa nchini kipo
katika kituo kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam na
kinafanya kazi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu na mfumo wa
utambuzi wa eneo (GPS) ambapo askari polisi waliopo katika kituo cha
mawasiliano watakuwa wakipokea simu kutoka kwa wananchi wanaotoa taarifa
za matukio ya uhalifu na kisha kuwaelekeza askari walio jirani ili
wafike eneo la tukio na kukabiliana na wahalifu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu
amemueleza Rais Magufuli kuwa kituo hicho kina uwezo wa kupokea simu 18
kwa mpigo kutoka kwa watu wanaopiga simu ya bure namba 111 au 112 kwa
ajili ya kutoa taarifa za uhalifu na kwamba lengo la jeshi hilo ni
kuhakikisha askari wanafika eneo la tukio ndani ya dakika 15.
IGP Mangu ameongeza kuwa kituo hicho kimeanzishwa kwa msaada kutoka
benki ya CRDB iliyotoa shilingi milioni 320, kitaanza kutoa huduma
tarehe 01 Julai, 2016 kikianzia katika mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni
Kanda maalum ya Dar es salaam na polisi imejiwekea malengo ya kuwa na
vituo kama hivyo nchi nzima ifikapo mwaka 2019.
Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho, Rais Magufuli
amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuanzisha mradi huo na ameahidi kuwa
serikali itahakikisha inaunga mkono mpango huo ikiwa ni pamoja na
kulifanyia kazi ombi la kununuliwa helkopta itakayorahisisha zaidi
ufikaji eneo la tukio.
Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi kuwanyang’anya silaha
wahalifu kabla hawajawadhuru raia na kupora mali zao ama kusababisha
mauaji, na amewataka viongozi wa jeshi hilo kuwazawadia askari
wanaofanya kazi nzuri ya kupambana na wahalifu.
Dkt. Magufuli pia ametaka jeshi la polisi lisimame imara kuhakikisha
serikali inatekeleza ahadi zake kwa wananchi zikiwemo upatikanaji wa
maji na huduma nyingine za kijamii na kwamba hatarajii kuona mtu yeyote
anafanya vitendo vitakavyosababisha ahadi hizo kutotekelezwa.
Post your Comment





