Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania
imesema kuwa imejipanga kupambana na ugonjwa wa homa ya manjano kwa
kuandaa timu za wataalam, vifaa tiba na chanjo za kutosha kuweza
kukabiliana na ugonjwa huo endapo utajitokeza nchini.
Msemaji wa Wizara Nsachris Mwamwaja amesema pamoja na jitihada za
serikali ni vyema wananchi wenyewe wakajitokeza mapema hospitali pindi
wanapobaini kuwa na dalili za ugonjwa wa homa ya ini.
Mlipuko wa homa ya manjano umesababisho vifo vya watu 138 nchini
Angola, na nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako ugonjwa
huo umeripotiwa kuuwa watu kadhaa, na nchini Kenya mtu mmoja amefariki
dunia.
Mwamwaja ametaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kutokwa na
damu sehemu za wazi kama mdomoni, pua, macho na tumboni na wakati
mwingine damu huonekana kwenye matapishi na kinyesi na baadaye figo
kushindwa kufanya kazi.
Dalili nyingine ni maumivu ya misuli pamoja na mgongo, mwili
kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kusikia kichefuchefu na kutapika,
mwili kuwa na manjano ambapo amewataka wananchi kuzingatia usafi ili
kuondoa uwezekano wa mazalia ya mbu waenezao ugonjwa huo.
Post your Comment




