WAKATI siku 21 zilizotolewa kwa benki zilizokuwa zikitumika kuweka
mishahara ya watumishi hewa zikiwa zimeisha jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda amesema ameshapata taarifa alizohitaji kutoka
katika benki hizo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Makonda alisema benki hizo
zimeshapeleka taarifa ingawa aliahidi kutoa ufafanuzi zaidi baada ya
kukaa na kuzipitia. Makonda alitoa siku hizo 21 zilizoisha jana, benki
hizo kurejesha fedha hizo serikalini au zitaje watu waliokuwa wakitumia
akaunti husika.
Alichukua hatua hiyo baada ya Mkoa wa Dar es Salaam kuwa na ongezeko
kubwa la watumishi hewa ambao fedha walizokuwa wanalipwa zilikuwa
zinapita katika benki husika. Mpaka sasa, mkoa wa Dar es Salaam
umebainika kuwa na watumishi hewa 283, ambao wanadaiwa kuisababishia
serikali hasara ya Sh bilioni 3.6 ambazo zilitumika kuwalipa mishahara.
Makonda alisema benki ndio pekee wanaoweza kusaidia mkoa, kutambua
wahusika waliokuwa wanatumia akaunti hizo pamoja na wale waliokuwa
wanachukua fedha hizo. Alitaja benki hizo na fedha zilizoko ni NMB yenye
Sh bilioni mbili, CRDB zaidi ya Sh milioni 400, NBC zaidi ya Sh milioni
141, DCB Sh milioni 85, Standard Chartered zaidi ya Sh milioni mbili na
Community Benki zaidi ya Sh milioni 100.
“Hakuna mtu anayeweza kutumia akaunti ya mtu bila kufuata taratibu za
kibenki, hata kama mtu amefariki kuna taratibu za kufuata ndipo apate
akaunti, naamini benki hizi zitasaidia kuwatambua wahusika wote,”
alisisitiza.
Wakati huo huo gazeti hili lilizungumza na wasemaji wa baadhi ya
benki hizo ambao wengi walisema mwenye uwezo wa kutolea ufafanuzi ni
Mkuu wa Mkoa. Meneja Uhusiano wa NMB, Vicent Mnyanyika alisema wao kama
benki hawawezi kusema chochote ni vyema suala hilo likatolewa ufafanuzi
na Makonda ambaye ndio aliyeagiza kama amepata mrejesho kutoka katika
benki hizo.
Kwa upande wa CRDB, Meneja Uhusiano wa Benki hiyo, Godwin Semunyu
alisema, Mkurungenzi Mtendaji wa benki hiyo ndiye atatolea ufafanuzi.
Post your Comment



