WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema sukari haitakuwa tatizo katika
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na wakuu wa mikoa wamepewa maelekezo kilo
moja isizidi Sh 2,300. Alisema hayo jana wakati wa mahojiano na
waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Miaka Mitano uliofanyika Chuo cha Mipango mjini hapa.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema alisema hadi Mei 13, mwaka huu walikuwa
wamepokea tani nyingine 35,000 za sukari na haitakuwa tatizo kwa kuwa
tayari jitihada kuwa serikali imefanya katika kushughulikia suala hilo.
Pia alisema sukari nyingine tani 11,000 imeshatoka na inasambazwa na
nyingine tani 20,000 iko tayari Tanzania na tani nyingine 35,000
zinakuja kabla ya Juni 30, mwaka huu. Alisema sukari wameigawa kwa kanda
kutokana na kanda kutofautiana kulingana na wingi wa watu kwa mujibu wa
mgawo wa Bodi ya Sukari Tanzania wamepeleka maeneo yote.
“Niwasihi Waislamu wenzangu ambao wamefunga Ramadhani kwamba suala la
sukari halitakuwa tatizo,” alisema. “Mwito wangu kwa wafanyabiashara
kuwa waaminifu na kutambua sukari ni mahitaji ya Watanzania wote.”
Alisema suala la bei wameangalia kule juu wanaponunua Brazil,
Uarabuni na Malawi wameshaweka viwango vya bei ambavyo wakuu wa mikoa
wataangalia sukari haitazidi Sh 2,300 kwa kilo ili Watanzania wote
wamudu kununua.
Alitoa mwito kwa wafanyabiashara kuacha kuficha sukari kwani hayo ni
mahitaji ya wananchi wote na hawana sababu ya kufanya hivyo. Katika
miezi ya karibuni, sukari ambayo ni moja ya bidhaa muhimu nchini,
imepanda bei hadi kuuzwa kati ya Sh 2,500 hadi 3,000 kwa kilo kutoka Sh
takriban 1,800, hali iliyosababisha serikali kuingilia kati kuwataka
wafanyabiashara kuuza kilo moja kwa Sh 1,800 na kuagiza sukari kutoka
nje ili kukabili upungufu uliopo.
Post your Comment


