MWANAMUZIKI Nguza Vicking ‘Babu
Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ ambao wanasota jela kwa
kosa la kuwanajisi watoto 9, wamedaiwa kusaka uwezekano wa kujinasua
gerezani kwa kumuangukia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
John Pombe Magufuli.
Taarifa kutoka kwa chanzo makini
zimeeleza kuwa wanamuziki hao kwa kushirikiana na ndugu zao,
wamemuandikia barua binafsi Rais ili aweze kusikia kilio chao na
ikiwezekana wasamehewe kutokana na mamlaka aliyo nayo.
“Si unakumbuka kipindi kile waliwahi
kumuandikia waraka JK (Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya nne) kumuomba
awasamehe lakini bahati mbaya maombi yao hayakuzaa matunda! Wameona
wajaribu kwa Magufuli ili ikiwezekana kupitia ile sheria inayompa
mamlaka rais kusamehe mtu yeyote aliyehukumiwa kwa kosa lolote,
awasamehe kina Babu Seya,
“Nasikia wameshaandika barua,
wanaipeleka ikulu na wana imani Magufuli ni mtu anayeguswa sana na hofu
ya Mungu, huenda akawasamehe,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa mtoto mkubwa wa Babu Seya,
Mbangu Nguza na kuulizwa kama wamepeleka barua hiyo na matumaini ya
ndugu zake kutoka gerezani, hakutaka kukubali au kukataa lakini akasema
wao wana imani muda wowote ndugu zao watatoka gerezani.
“Kila siku nimekuwa nikisisitiza hili
suala, labda niseme tena, Babu Seya na Papii watatoka siku si nyingi
kutoka sasa,” alisema Mbangu.
Chanzo chetu kiliwasiliana na Kaimu Mkurugenzi
wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa na kumuuliza kama wamepokea barua
hiyo, alisema hawajaipata na kuomba apewe muda afuatilie na atatoa
majibu.
“Sijaiona hiyo barua, ngoja nitafuatilia na nitakujulisha,” alisema Msigwa.
KUMBUKUMBU
Juni 25, 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa
Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Addy Lyamuya aliwatia hatiani Babu
Seya na wanaye watatu, Papii Kocha, Mbangu na Francis.
Januari 27, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao
iliyokuwa ikipinga hukumu hiyo.
Wakili wao, Mabere Nyaucho Marando
akapeleka suala hilo Mahakama ya Rufaa Tanzania ambako Mbangu na Francis
waliachiwa huru, Babu Seya na Papii wakaonekana bado wana hatia.
Babu Seya na wanaye walidaiwa kutenda
makosa 10 ya kubaka na kulawiti watoto hao kati ya Aprili na Oktoba,
2003 katika maeneo ya Sinza ya Palestina, Dar es Salaam. Mpaka sasa wana
miaka 12 gerezani.
Post your Comment


