Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kulitaka
Baraza la Vijana la Chama hicho (BAVICHA) kusitisha mpango wao wa
kukutana Dodoma kuzuia kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, Baraza
hilo limetangaza mtindo mwingine wa kuingia mjini hapo.
Mwenyekiti
wa BAVICHA, Patrobas Katambi amesema kuwa Baraza hilo limepanga kufanya
mkutano wake wa Kamati ya Utendaji kuanzia Julai 20 mwaka mjini Dodoma
kwa lengo la kujadili muelekeo wa Demokrasia nchini.
“Kikao chetu
cha Kamati ya Utendaji tulikuwa tumekiahirisha baada ya polisi kuzuia,
lakini sasa tunafanya tena kwa tarehe ileile ambayo ni Julai 20 mjini
Dodoma ambapo tulipanga kufanya mwanzo,” Patrobasi Katambi aliwaambia
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Aidha, amewataka vijana
wa chama hicho nchi nzima kuendelea kuwa watulivu na kutii agizo la
Mwenyekiti wa chama hicho la kutoingilia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM
ambao utafanikisha kumkabidhi Rais John Magufuli Uenyekiti wa chama
hicho, Julai 23.
Patrobas alilitupia lawama Jeshi la Polisi kwa
kuruhusu kufanyika kwa mkutano huo wa CCM akisema kuwa inaonesha
kushindwa kusimamia utekelezaji wa amri zake. Alidai kuwa Mkuu wa Jeshi
hlo, IGP Ernest Mangu anapaswa kujiuzulu endapo ataruhusu kufanyika kwa
mkutano huo.
Hivi karibuni, Jeshi la Polisi liliwakamata na
kuwafikisha mahakamani viongozi wa BAVICHA waliokuwa mjini Dodoma
akiwemo Mwenyekiti wake, kwa tuhuma za kutaka kuhamasisha vurugu na
kuvaa fulana zenye maandishi yanayolenga kuikashfu Serikali. Viongozi
hao wako nje kwa dhamana.
Post your Comment