Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi kwa Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia
kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Kilindi Mkoani Tanga Mhe. Beatrice
Shelukindo kilichotokea jana tarehe 02 Julai, 2016.
Mhe. Beatrice Shelukindo ambaye amewahi kuwa Mbunge Bunge la Afrika
Mashariki na baadaye kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa vipindi viwili mfurulizo hadi alipostaafu mwaka jana 2015,
amefariki dunia akiwa nyumbani kwao Njiro Mkoani Arusha.
Katika salamu zake Rais Magufuli amesema taifa limempoteza mtu
aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo hususani alipokuwa Mbunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwawakilisha wananchi wa
Jimbo la Kilindi na Mkoa wa Tanga.
“Mhe. Beatrice Shelukindo alikuwa kiongozi shupavu,
ambaye siku zote alisimama kidete kupigania maendeleo ya wananchi na
kutetea rasimali za taifa.
“Kupitia kwako Mhe. Spika Job Ndugai naomba unifikishie
salamu zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote wa
marehemu na pia kwa wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Amesema Rais Magufuli.
Dkt. John Pombe Magufuli pia amewaombea wote walioguswa na kifo cha
Mhe. Beatrice Shelukindo kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika
kipindi hiki cha kuondokewa na mpendwa wao na amemuombea marehemu
apumzishwe mahali pema peponi, amina.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
03 Julai, 2016
Post your Comment



