Duru ya pili ya mazungumzo kusaka maridhiano nchini Burundi yanatarajiwa kuanza Jumanne Julai 12 hadi Julai 14, 2016.
Taarifa iliyotolewa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,
EAC, imesema mazungumzo hayo yatafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa
Kimataifa Arusha, AICC, chini ya muwezeshaji wake, Rais Mstaafu wa
Tanzania, Benjamin William Mkapa.
Tayari Mh. Mkapa amekwishakutana na Marais wastaafu wa Burundi,
viongozi wa vyama vya siasa, dini, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja
na kufanya mashauriano na masuluhisho wa mgogoro wa Burundi, Rais
Yoweri Museveni wa Uganda .
Katika mazungumzo yake na wadau hao, masuala muhimu kadhaa yaliibuka
ikiwemo utekelezaji wa makubaliano ya Arusha ya amani na maridhiano ya
Burundi, Katiba ya Burundi, hali ya usalama, nafasi ya siasa na
demokrasia, hali ya uchumi na pia mchango wa nchi wanachama wa EAC na
nchi nyingine jirani katika mazungumzo hayo.
Hivyo, duru ya pili ya mazungumzo itajikita zaidi katika kufikia
makubaliano ya pamoja kwa ajili ya kuleta utengamano, maendeleo na
mustakabal wa Burundi.
Post your Comment


