Polisi wenye silaha hivi
karibuni walifika nyumbani kwa msanii nyota, Nasibu Abdul ‘Diamond
Platnumz’ anayeishi Mivumoni Madale na kusitisha shughuli za burudani
zilizokuwa zikiendelea ndani.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika,
shughuli iliyositishwa na polisi ilikuwa ni ile ya kusherehekea siku ya
kuzaliwa ya mama mzazi wa mkali huyo wa muziki, Sanura Kassim ‘Sandra’
iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita. Ilidaiwa kwamba msanii huyo
amekuwa akifanya sherehe mara kwa mara katika nyumba yake hiyo, hali
inayosababisha kero kwa baadhi ya majirani zake, ambao nao, wamekuwa
wakilalamika mara kwa mara kwa viongozi wa serikali ya mtaa huo.
Chanzo chetu baada ya kuupata ubuyu huo,kilifunga safari hadi nyumbani kwa msanii huyo na kufikia ofisini kwa
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mivumoni, Deodatus Kamugisha ambaye
baada ya kuulizwa kuhusu kuwepo kwa tukio hilo la askari kuzima sherehe
hiyo, alikiri kuwa ni kweli.
“Nimekuwa nikipata malalamiko ya mara
kwa mara kuhusu sherehe za Diamond kuwa waalikwa wake ni vijana wa
kihuni ambao wakija huwa wanavuta bangi hadharani, wanafunga barabara
pamoja na kujisaidia haja ndogo hovyohovyo maeneo ya nje ya nyumba yake.
“Juzi nilipigiwa simu usiku na majirani
zaidi ya sita wakila lamika kuhusu sauti kubwa ya muziki wa kwenye
sherehe ya Diamond, nilimuita lakini akakaidi, ikabidi niende Kituo cha
Polisi cha Wazo na kuchukua polisi wakiwa na silaha na kwenda kufunga
sherehe ile, sheria iko wazi kuhusu utaratibu wa kupiga muziki maeneo ya
baa na majumbani,” alisema Kamugisha.
Baadhi ya majirani waliozungumza nasi, walisema kumekuwa na tabia ya Diamond kufanya sherehe mara
kwa mara nyumbani hapo, huku muziki mkubwa ukipigwa, jambo ambalo kwao
ni kero.
“Nachukizwa sana na kelele za Diamond,
kwani watu tunashindwa kulala kwa sababu yeye anafanya sherehe mbona
kuna kumbi na hoteli anaweza kwenda tu, mimi nyumba yangu ni kama
kilomita mbili kutoka kwake, lakini nasikia muziki kwa kero, je walio
ubavuni mwake si wanataabika sana!” alisema mzee mmoja aliyeomba hifadhi
ya jina lake.
Chanzo chetu kilimtafuta Diamond kwa simu yake mkononi ili kuzungumzia ishu hiyo lakini iliita bila kupokelewa kwa muda wote.
Post your Comment




