Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefungua duka la Bohari Kuu ya Dawa
(MSD) katika Hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambalo litakuwa
na uwezo wa kuhudumia hospitali 524 katika mikoa ya Lindi, Mtwara na
wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Akizindua duka hilo leo
(Jumamosi, Julai 16, 2016) Waziri Mkuu amesema duka hilo litaendelea
kuboresha huduma za upatikanaji wa dawa kwa gharama nafuu katika
hospitali, vituo vya afya na zahanati katika wilaya ya Ruangwa pamoja na
mikoa na wilaya za jirani.
Duka hilo ni la sita kufunguliwa tangu
Mhe. Rais Dk. John Magufuli alipotoa agizo kwa MSD kufungua duka la
dawa ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambapo mengine yako
katika mikoa ya Mwanza (Sekou Toure), Arusha (Mount Meru), Mbeya (karibu
na hospitali ya mkoa) na Geita (hospitali ya wilaya ya Chato).
“Duka
hili litasaidia kufikiwa kwa malengo ya Serikali ya kuboresha huduma za
afya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba
kwa wakati na kwa gharama nafuu, hivyo nawaomba mlitumie duka hili,”
amesema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa
benki ya NMB, kikosi cha SUMA JKT na MSD kwa kufanikisha ujenzi wa duka
hilo ambalo litaimarisha upatikanaji wa dawa kwa uharaka.
Awali
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema kuanzishwa kwa duka
hilo kutaongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa gharama nafuu ,
hivyo kuondoa usumbufu kwa wagonjwa wa kwenda kuzitafuta katika ya
mbali na kwa bei kubwa.
“Nitoe mfano wa tofauti wa bei za dawa
kati ya maduka yetu na mengine, dawa ya sindano ya diclofenac tunauza
sh. 250 huku mitaani ni sh. 1,000 hadi 1,500 , ampliclox dozi moja MSD
sh. 1,500 mtaani sh. 3,500 na Ciprofloxacin MSD sh. 100 na mtaani sh.
500 hadi 1,000,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema lengo la maduka
hayo si kuuza dawa reja reja, nia yao ni kuziuzia hospitali, vituo vya
afya na Zahanati ili wagonjwa wanapokwenda huko kupatiwa huduma wasikose
dawa kwa wakati.
Akizungumzia kuhusu gharama za ujenzi wa duka
hilo Bwanakunu mesema umegharimu sh.milioni 59 ambapo kati yake MSD
imetoa sh. milioni 29 na benki ya NMB imetoa sh. milioni 30.
“Mbali
na gharama za ujenzi MSD tumenunua na kufunga vifaa vya TEHAMA kwa sh
milioni 17 na mtaji wa dawa wa sh. milioni 37, ambapo imetenga sh.
milioni 100 kwa ajili ya dawa za duka hilo.
Amesema duka hili
litaendeshwa na kusimamiwa na MSD kwa muda wa mwaka mmoja na kisha
wataikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa ajili ya kuliendeleza
ambapo litaisaidia katika kuiongezea mapato.
Post your Comment



