Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Kampuni ya Udalali
ya Yono, wameifungia Kampuni ya Benchmark Productions na kuipa muda wa
siku 14, iwe imelipa deni la kodi ya Sh bilioni 7.04, vinginevyo mali za
kampuni hiyo zitauzwa kwa mnada.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Meneja Msaidizi wa Madeni wa
TRA, Mkoa wa Kinondoni wa Kodi, Sylver Rutagwelera alisema wamefikia
hatua hiyo baada ya kuidai kampuni hiyo inayomilikiwa na Rita Paulsen
kwa muda mrefu bila kulipa.
TRA, wakiwa na Kampuni ya Udalali ya Yono, walifika eneo la Mikocheni
jijini hapo jana asubuhi ziliko ofisi za kampuni hiyo na kuwaeleza
wahusika kuhusu deni hilo, na kuwataka waoneshe risiti za malipo iwapo
wameshaanza kulipa deni hilo, jambo ambalo wahusika hao hawakuwa nazo.
Hata hivyo Meneja Operesheni wa Kampuni hiyo aliyejulikana kwa jina
moja la Evelyn alifika ofisini hapo na kuwaambia maofisa hao kuwa
walishaanza mawasiliano jinsi ya kulipa deni hilo. “Zipo barua
tulizokuwa tumeanza kufanya mawasiliano na TRA, kuhusu deni hili, lakini
pamoja na hayo, deni lenyewe ni kubwa kuliko uwezo wa kampuni,” alisema
Evelyn.
Hata hivyo Rutagwelera alisema mmiliki wa kampuni hiyo anadaiwa kodi
tangu mwaka 2009 na alikuwa akitumia jina lingine kwenye kampuni hiyo na
baada ya muda aliifunga na kufungua hiyo ya Benchmark ili hali deni la
nyuma hajalipa.
“Mdaiwa huyo alikuwa ana kampuni aliyoipa jina lingine na
tulimkumbusha kulipa kodi ya serikali tangu mwaka 2009 ila hakutekeleza
na badala yake aliamua kuifunga kampuni na kufungua hii, akidhani deni
limefutika”, alisema Rutagwelera.
Alisema baada ya kuona muda unasonga na deni linazidi kuongezeka bila
mdaiwa kuonesha juhudi za kulipa waliamua kukabidhi mdaiwa huyo kwa
Kampuni ya Yono kwa ajili ya kufuatilia deni hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Yono, Scholastika Kevela
alisema wameifungia kampuni hiyo na kuanzia sasa walinzi wa Yono
watalinda na baada ya muda wa siku 14, waliopewa kulipa deni hilo
ukipita, watachukua hatua nyingine kisheria ya kuuza mali za kampuni
hiyo kwa mnada.
Alisema deni hilo ni kubwa kwa sababu ni muda mrefu umepita kodi ya
serikali haijalipwa na kuwashauri Watanzania kuacha tabia ya kulimbikiza
kodi kwa sababu deni litakuwa kubwa ila likilipwa kwa wakati linaondoa
usumbufu usio wa lazima.
“Yono tumepewa kazi ya kukusanya madeni ya serikali na tutaendelea
kuwakamata wale wote tunaopewa kuwafuatilia lengo sio kuwaumiza ni
kuhakikisha kodi ya serikali inakombolewa kwa manufaa ya nchi yetu, kwa
maana tunamuunga mkono Rais John Magufuli kuhakikisha taifa letu
linaendelea kwa kukusanya mapato stahiki”, alisema Kevela.
Kevela alisema kazi ya kuendelea kukusanya madeni kwa wadaiwa wengine
wa serikali inaendelea na sasa wako kwenye hatua mbalimbali za
ukusanyaji ikiwa ni pamoja na kuendesha mnada wa mali za wadaiwa
mbalimbali ili kupata fedha za serikali.
Post your Comment



