
Mheshimiwa Balozi Peter A. Kallaghe amewasilisha rasmi barua yake ya utambulisho (Letter of Credence) kwa Mheshimiwa Rais wa Ireland Michael Higgins katika sherehe fupi iliyofanyika katika Ikulu ya nchini hiyo jijini Dublin.
Pamoja na barua hiyo Balozi Kallaghe aliwasilisha rasmi salamu za Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikimtakia Rais Higgins afya njema na furaha.
Nae Rais Higgins alipokea salamu hizo kwa kusifu uhusiano wa kihistoria kati ya nchi hizi mbili. Alimkumbuka Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere kama mtu shupavu aliyeijengea Tanzania misingi thabiti ya kisiasa na kiuongozi. Aidha alikumbuka uzuri wa Tanzania na wananchi wake, alioushuhudia alipotembelea Kilosa, mkoani Morogoro miaka ya 1980.
Katika shughuli hiyo Balozi Kallaghe alisindikizwa na Mkewe Joyce na Afrisa wa Ubalozi Amos Msanjila. Pamoja na kuiwakilisha Tanzania, Uingereza, (United Kingdom) Ubalozi wa Tanzania London unaiwakilisha nchi pia huko Ireland. Tanzania ni moja ya nchi saba tu zinazopata misaada ya kimaendeleo toka Ireland, hasa kupitia taasisi yao ya Irish Aid. Nchi zingine ni Ethiopia, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Uganda na Zambia.

Post your Comment