
MSAFARA wa Rais Jakaya Kikwete umepata ajali baada ya mmoja wa walinzi wake kuteleza na pikipiki na kuanguka katika eneo la kituo cha daladala cha Kibo jijini Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 5 asubuhi wakati Rais Kikwete, akielekea kwenye msiba wa mmoja wa madereva wa Ikulu, Deokalyus Makwasinga, aliyefariki mwishoni mwa wiki eneo la Kimara Bucha.
Baada ya ajali hiyo, msafara wa Rais ulisimama kwa muda na ujumbe wake kuteremka kumsaidia majeruhi huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha tukio hilo, akisema kuwa askari polisi huyo wa kikosi cha usalama barabarani, alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.
Kenyela alisema ajali hiyo ilichangiwa na mvua ya manyunyu iliyokuwa ikinyesha muda huo na kusababisha pikipiki hiyo kuteleza.
Alimtaja askari aliyepata ajali kuwa ni mwenye namba D7380 Sajenti Steven Raiza, ambaye aliteguka bega na kupata michubuko sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Ni bahati mbaya tu na imechangiwa na tuta pamoja na rasharasha ya mvua iliyosababisha kuteleza kwa pikipiki hiyo,” alisema.
Hata hivyo, Kenyela alisema kuwa hali ya askari Raiza inaendelea vizuri baada ya kupata matibabu.
Chanzo: Tanzania Daima
Post your Comment


