SERIKALI imewatoa wasiwasi Watanzania kuhusu taarifa za kutokea kwa
uhaba wa mafuta ya ndege, uliokuwa ukitishia kusimama kwa usafiri huo
muhimu kwa nchi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema hayo
bungeni jana jioni wakati alipokuwa akihitimisha mjadala wa Bajeti ya
wizara hiyo, alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe
Zitto (ACT-Wazalendo).
Awali Zitto katika hoja yake, alisema kuwa akiba ya mafuta ya ndege
nchini imebaki ya siku tano, jambo linaloweza kusababisha ndege za
kimataifa kushindwa kutua nchini.
“Zimebaki siku tano mafuta ya ndege aina ya JET AI kumalizika nchini
baada ya mafuta yote kugundulika kuwa yamechafuka. Sasa baada ya siku
hizo, ndege hazitatua nchini na itakuwa ni aibu na nchi itakosa fedha za
kigeni kwa watalii kutokuja nchini,” alisema Zitto.
Alisema anazo barua kutoka kwa Wakala wa Kuagiza Mafuta kwa Pamoja na
alikuwa tayari kuziwakilisha kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo. Uchunguzi Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili,
ulibainisha kuwa kuna mafuta ya siku 15.
Taarifa kutoka vyanzo vinavyohusika na upokeaji wa mafuta nchini,
hadi kufikia jana akiba ya mafuta ya ndege JET AI yanayofaa kwa matumizi
ilikuwa lita 8,749,810 wakati yale ambayo ubora wake haufai, yalikuwa
lita 28,131,341.
Taarifa hiyo ilionesha kuwa Puma Energy Tanzania ina lita 4,596,391,
Oilcom (T) Ltd lita 256,842, Total (T) Ltd lita 2,715,516 na Gapco (T)
Ltd lita 1,181,061. Kati ya lita 28,131,341 zenye ubora usiofaa, lita
14,432,736 zipo Puma Energy Tanzania, lita 10,840,059 ziko Oilcom (T)
Ltd na lita 2,858,546 ziko Gapco (T) Ltd.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, matumizi ya mafuta ya ndege kwa siku ni
lita 571,484, hivyo mafuta yaliyopo kutosheleza kwa siku 15 kuanzia
jana. Aidha, ilifahamika kwamba mafuta ya ndege hayo aina ya JET AI
yanayofaa kwa matumizi yanayosafirishwa kwenda kwa SP Rwanda ambayo yako
katika ghala la Gapco ni lita 3,474,781.
Taarifa ya Waziri Akitoa majibu ya Serikali, Profesa Muhongo alisema
mafuta yaliyopo yanatosha kwa siku 16 na tahadhari zote zimechukuliwa,
kuhakikisha yataendelea kuwepo mpaka hapo shehena nyingine ya mafuta
hayo itakapoingia katikati ya Junei mwaka huu.
Alisema wakati tahadhari hizo zikiwa zimechukuliwa, Shirika la
Viwango (TBS), limeanza kufanya uchunguzi wa kilichotokea katika shehena
ya mafuta yaliyochafuka, kwa kuwa yaliagizwa kwa pamoja lakini ajabu
baadhi yalikutwa machafu na mengine masafi, huku akimwambia Zitto kuwa
aliyempa taarifa, ni mmoja wa wenye mafuta machafu.
Mchango wa Zitto Katika mchango wake mwingine, Zitto alitaka
kuongezwa kwa nguvu katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini,
akisema kuna tatizo la kampuni kubwa kutumia njia za kihasibu
kuhamasisha kwenda kule zilikosajiliwa.
Alitaka pia kuwapo kwa uangalifu katika kushughulikia mikataba ya
uzalishaji umeme ili kuepuka taifa kuja kulipa fedha nyingi kama
ilivyokuwa kwa Kampuni ya Dowans. Pia alipendekeza kuwapo kwa mapitio ya
sheria ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ili isaidie
kukusanya mapato zaidi katika madini.
Alishauri suala la mafuta na gesi kutokuwa la Muungano, kurekebishwa
katika sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu
bado halijafanyika hivyo, licha ya Zanzibar sasa kuwa
tayarikushughulikia masuala hayo kama nchi.
Mjadala wa vinasaba Katika hatua nyingine, Mbunge wa Manonga, Seif
Gulamali (CCM), amewataka wabunge watangulize mbele maslahi ya Taifa,
baada ya kuibuka kwa taarifa zilizosambazwa kwa wabunge kupinga matumizi
ya vinasaba,vinavyosaidia kutenganisha mafuta yanayosafirishwa kwenda
nje ya nchi, ambayo hayalipiwi kodi na yanayotakiwa kutumika nchini,
ambayo hulipiwa kodi.
Alitoa kauli hiyo baada ya kuibuka kwa hoja za wabunge wakipinga
vinasaba hivyo wakitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura),
kuviondoa huku wengine wakitetea viendelee kuwepo.
Post your Comment



