MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Mlowa
wilayani Iringa, Eva Tolage (16) ambaye mwaka jana alimwandika barua
Rais Barack Obama wa Marekani akielezea kero zinazowakabili watoto wa
kike katika kijiji chake, juzi alitembelea bungeni mjini hapa, huku
akiwasisitiza viongozi wa kisiasa kuwajibika kwa kutekeleza ahadi zao
ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi.
Eva aliyepata pia fursa ya kukutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
na viongozi mbalimbali alisema jambo hilo hakulitarajia, kwani wakati
anaandika barua hiyo hakufahamu kuwa itamfikia Rais Obama na kujibu.
Alisema viongozi wa kisiasa wana wajibu mkubwa wa kusimamia ahadi zao
ili kuondoa kero vijijini hasa upatikanaji wa maji. Akizungumza wakati
wa mahojiano na waandishi wa habari, alisema kero ya maji ni kubwa
kijijini kwao ambapo watu na mifugo wamekuwa wakichangia maji.
“Maji ni adimu shuleni, yanapopatikana hadi kijijini kwetu ni
kilometa saba hali inayofanya wasichana waishi katika mazingira
hatarishi zaidi. Unaweza kupata vishawishi vya wavulana njiani na
ukajikuta umepata ujauzito na kushindwa kuendelea na shule.
“Niliamua kumuandikia barua Rais Obama ili atusaidie kupata maji,
nilipoandika barua hiyo nikawapatia Shirika la Health Development,
lakini nilipopata taarifa kuwa barua hiyo imemfikia Rais Obama nilisikia
furaha kwani ni jambo la ajabu sikulitegemea,” alisema.
Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mlowa, anakosoma Eva, Denis
Myovela alisema wamefurahishwa na ujasiri wa mtoto huyo na wanategemea
shule yao itapata maji.
Meneja wa kampeni ya Simama na Eva, Oscar Kimario alisema barua
iliyoandikwa na Eva ilisomwa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa na Rais
Obama akihimiza viongozi kutekeleza majukumu yao.
Eva aliandika barua baada ya kumaliza elimu ya msingi akiwa na miaka
15 wakati wa ukimalizika utekelezaji wa Mpango wa Malengo ya Milenia
(MDGS) na Rais huyo akaijibu katika mkutano wa 70 wa Baraza la Umoja wa
Mataifa wa Septemba, mwaka jana uliojadili Maendeleo Endelevu ya Dunia.
Post your Comment



